Bazara la Sanaa la Taifa (BASATA) limeandaa mafunzo maalumu ya kuwajengea uwezo wasimamizi na waendeshaji wa matukio nchini kama hatua ya kuwajengea uelewa wa namna ya kufanya shughuli zao kwa kuzingatia sheria za nchi ili waweze kukuza ubora na viwango vya kitaalamu katika sekta ya matukio.
Mafunzo haya yanalenga kuwafikia wadau mbalimbali, wakiwemo Watangazaji na Waongozaji wa Matukio (MCs), Maafisa Utamaduni, Maafisa Habari, Promota, kampuni zinazojihusisha na uandaaji na usimamizi wa matukio pamoja na wadau wengine katika sekta hiyo.
Akizungumza na waandishi wa Habari jana jijini Dar es Salaam, Kaimu Katibu Mtendaji wa BASARA, Amosi Mazaba, alisema mafunzo hayo yatafanyika tarehe 23 – 24 Novemba 2026 katika ukumbi wa The East Africa Commercial and Logistics Centre (EACLC), Ubungo, Dar es Salaam. Iliyokuwa standi ya Mabasi ya Mikoani Ubungo.
Aidha, alisema mafunzo haya ni sehemu ya jitihada za BASATA za kuimarisha weledi, ujuzi na mifumo ya uendeshaji na usimamizi wa matukio nchini, sambamba na kukuza ubora na viwango vya kitaalamu katika sekta ya matukio.
“Uamuzi wa kuandaa mafunzo haya umetokana na kukua kwa kasi kwa sekta ya matukio nchini, ikiwemo matamasha, maonesho ya sanaa, matukio ya muziki, burudani na shughuli mbalimbali za kijamii na kitaasisi. Ukuaji huu unaonesha umuhimu wa kuwa na wataalamu wenye ujuzi wa kutosha katika kupanga, kuratibu, kuendesha na kusimamia matukio kwa kuzingatia sheria, kanuni, maadili na viwango vinavyokubalika,” alisema.
Alisema kupitia mafunzo hayo, BASATA inalenga kuongeza ujuzi na weledi wa washiriki, kuimarisha uratibu na usimamizi wa matukio, kuongeza uelewa wa sheria na miongozo inayosimamia shughuli hizo, pamoja na kuwajengea uwezo wa kutambua, kuzuia na kukabiliana na changamoto zinazoweza kujitokeza wakati wa utekelezaji wa matukio.
Naye Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Ukuzaji Maendeleo ya Sanaa wa BASATA, Lilian Shayo alisema BASATA inaamini kuwa mafunzo hayo yatasaidia kuongeza ubora wa matukio, kuimarisha usalama wa wasanii na washiriki, kupunguza changamoto zinazoweza kuzuilika.
Aliseama mafunzo hayo yanatarajiwa kuongeza fursa za ajira na kujiajiri, pamoja na kukuza mchango wa sekta ya matukio katika uchumi wa ubunifu na maendeleo ya Taifa.
“BASATA inatoa wito kwa wadau wote wanaojihusisha na sekta ya matukio, taasisi za umma na binafsi kuwaunga mkono wataalamu wao kushiriki mafunzo haya ili kuongeza uwezo wao wa kitaalamu”.
“Baraza linaendelea kutekeleza jukumu lake la kukuza, kuratibu na kusimamia maendeleo ya sanaa nchini kwa kushirikiana na wadau mbalimbali, likiwa na dhamira ya kuhakikisha sekta ya sanaa na matukio inakuwa na tija, weledi na mchango mkubwa katika uchumi wa Taifa,”




