
Sehemu ya Hotuba ya Katibu Mkuu wa ACT Wazalendo Ado Shaibu aliyoitoa katika Kata ya Ruaruke, Jimbo la Kibiti, jana Septemba 15, 2024.
“Ndugu zangu Wana-Kibiti, ninafahamu kuwa wanamageuzi wengi wa Kusini na Pwani mlikiamini na kukipenda Chama cha CUF. Mliamini kuwa ajenda ya ukombozi, hasa wa kiuchumi kwa maeneo ya Kusini na Pwani itabebwa na CUF”-Ado
“Hali ya sasa, nyinyi nyote ni mashahidi, CUF imepoteza dira na inasubiri kuzikwa rasmi. Kwa yeyote ambaye aliiamini ile ‘haki sawa kwa wote’ na ‘ngangari’ bila shaka anajionea kwa macho kuwa CUF haina uwezo huo tena”-Ado
“Baada ya marehemu Maalim Seif Sharif Hamad kujiunga na ACT Wazalendo, Wana-CUF wengi ‘walishusha tanga’ kumfuata. Hatua hii, si tu kwamba ilikipa nguvu chama chetu, lakini pia ilibadili kabisa ramani ya kisiasa nchini. Upesi upesi, ACT Wazalendo kimekua kwa kasi sana” -Ado

“Tunajua kuna Wana-CUF wengi ambao mmekata tamaa na mageuzi baada ya kilichotekea mwaka 2019. Tunajua baadhi mmepunguza harakati na kujikita kwenye shughuli binafsi. Tunajua pia mpo ambao mna matumaini pengine CUF itafufuka. Binafsi sioni hilo likitokea” -Ado
“Rai yangu kwenu wapiganaji mliobaki CUF hapa Kibiti na Tanzania kwa ujumla, karibuni sana ACT Wazalendo tuendeleze mapambano. ACT Wazalendo ndio jahazi sahihi kwenu”-Ado
“Tutawapokea wote kwa mikono miwili na kwa pamoja tutaendeleza sera zilezile za haki sawa kwa wote ili kujenga ‘Taifa la Wote kwa Maslahi ya Wote’ na ‘Zanzibar Mpya, Zanzibar Moja Mamlaka Kamili”- Ado