Ancelotti asema Mbappe sasa ni mpya zaidi

CARLO Ancelotti alisifu uchezaji wa Kylian Mbappe baada ya fowadi huyo kufunga katika ushindi wa mabao 2-0 wa Real Madrid ugenini dhidi ya Real Sociedad Jumamosi, akisema anaonekana “mpya zaidi, mwenye bidii zaidi” na “anaimarika sana.”

Vinicius Junior alitangulia kufunga kwenye Uwanja wa Reale Arena dakika ya 58, kwa mkwaju wa penalti baada ya Sergio Gomez kuunawa mpira, kabla ya Mbappe kuongeza penalti nyingine dakika ya 75 Vinicius alipofanyiwa madhambi.

Katika mechi tano alizocheza Mbappe za LaLiga hadi sasa msimu huu, ana mabao matatu.

“Mbappe anaonekana mchanga zaidi, akifanya kazi zaidi kwenye mpira,” alisema Ancelotti katika mkutano wake na waandishi wa habari baada ya mechi.

“Ni hatari sana, ukichanganya vema na Vinicius na washambuliaji wengine. Anaimarika. Nilipenda mchezo wake sana.”

Ancelotti alisema amewaacha Vinicius na Mbappe kuamua nani apige penalti, huku wote wawili wakiwa wamefunga mara mbili kwenye kampeni hii.

“Kwanza ni Vini ndiye aliyefunga, kisha wakaamua Kylian achukue moja,” alisema Ancelotti. “Wanachukua jukumu, na hadi sasa imekwenda vizuri.”

Mbappe mwenyewe aliiambia Real Madrid TV kwamba anahisi anazoea mazingira yake mapya.

“Kila mchezo ninajisikia vizuri, ninaelewa kile timu, kocha na wachezaji wenzangu wanahitaji,” alisema Mbappe.

“Vinicius na mimi tunajaribu kutafutana kwenye mchezo na katika mazoezi ili kupata muunganisho huo, yeye ni mchezaji mzuri.

“Jambo muhimu ni kwamba penalti nne [hadi sasa msimu huu] zilikuwa mabao, si nani anayezifunga. Tulifunga zote nne, na hilo ndilo jambo muhimu zaidi.”

Leave a Comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *