Azam yaahidi kuendeleza ubabe mashindano Afrika

KOCHA Mkuu wa Azam FC, Yossoupha Dabo, amesema amekiandaa vyema kikosi chake ili kuhakikisha wanapata matokeo mazuri katika mechi ya marudiano ya mashindano ya kimataifa ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya wenyeji APR itakayochezwa kesho kwenye Uwanja wa Amahoro jijini, Kigali.

Katika mechi ya kwanza iliyochezwa wikendi iliyopita, Azam FC ilipata ushindi wa bao 1-0.

Dabo aliliambia gazeti hili amewaandaa wachezaji wake kisaikolojia kuhakikisha wanaenda kujituma katika mechi hiyo ya marudiano kwa sababu wanataka kusonga mbele kwenye michuano hiyo inayoandaliwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF).

Kocha huyo alisema amewaandaa wachezaji wake wasahau matokeo ya mechi ya kwanza na kuingia uwanjani kwa ajili ya kupambana kusaka ushindi.

Alisema anaamini mechi hiyo ya marudiano haitakuwa rahisi kwa sababu wapinzani wao watakuwa nyumbani ambapo pia wanahitaji matokeo mazuri yatakayowapeleka mbele.

“Tunaendelea na maandalizi, tunajua mechi hiyo inatarajiwa kuwa mgumu ingawa sisi tutaingia tukiwa na faida ya ushindi wa bao 1-0, hata hivyo hatutabweteka, tutajiimarisha na kufanyia kazi mapungufu yetu.

Hatutabweta, tumejipanga kufanya vizuri katika mashindano haya msimu huu, tunawaomba Watanzania waendelee kutuombea, hatutawaangusha,” alisema Dabo.

Alisema kila mchezaji ana morali ya kusaka ushindi na benchi la ufundi linaendelea kurekebisha makosa iliyobaini katika muda uliobakia.

“Nimekuwa na mazungumzo na wachezaji wangu kwa ajili ya kuwapa maelekezo ambayo wakiyafuata, nina hakika tutapata ushindi na kufikia malengo, lakini tutacheza kwa tahadhari wakati wote,” kocha huyo alisema.

Azam iliyomaliza katika nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu uliopita pamoja na mabingwa, Yanga wanashiriki mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika wakati Simba na Coastal Union zenyewe zinapeperusha bendera ya Bara kwenye michuano hiyo ya kimataifa.

Leave a Comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *