Wednesday, February 18, 2026
spot_img
HomeAfyaWasindikizaji wa wagonjwa JKCI walala nje kwa kukosa gharama za malazi

Wasindikizaji wa wagonjwa JKCI walala nje kwa kukosa gharama za malazi

Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), imesema iko mbioni kutafuta fedha za kujenga ‘nyumba ya matumaini’ kwaajili ya baadhi ya wanaosindikiza wagonjwa kwenye taasisi hiyo ambao baadhi yao wanalazimika kulala nje kwa kushindwa kumudu gharama za hoteli.

Hayo yamesemwa leo jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi wa Upasuaji wa JKCI, Angela Muhozya wakati wa hafla ya kuwashukuru waliochangia matibabu ya watoto kwenye taasisi hiyo wakati wa harambee ya mwaka jana.

Amesema JKCI inataka kujenga nyumba hiyo inayoitwa ya matumaini ili kuwapunguzia adha ya kulala nje wasindikizaji wa wagonjwa wanaotoka maeneo ya mbali kwani wengi wamekuwa wakilala nje ya hospitali hiyo kwa kushindwa kumudu gharama za hoteli.

“Unakuta mgonjwa akilazwa ndugu aliyemsindikiza hana pa kulala kwa hiyo wengi kwa kukosa hela ya kulala hotelini wanaamua kulala nje ya hospitali sasa JKCI kwa kushirikiana na Heart Team Foundation Africa tumefikiria kutafuta nyumba karibu na hapa kuwapa hifadhi ndugu wa wagonjwa, nyumba hii itawasaidia hata wagonjwa wetu tunapowaruhusu,’” alisema

“Kuna wagonjwa hapa tunawaruhusu lakini hawana ndugu hapa mjini sasa wengine wanapenda kukaa hapa hata mwezi kupumzika kwa hiyo wanakaa hapahapa hospitali kwa hiyo nyumba ya matumaini itakapopatikana watakuwa wanakaa hapo ingawa siyo bure kabisa watachangia kidogo sana kulinganisha na wanavyoweza kulipa hotelini,” alisema Dk Muhyoza

Awali, daktari bingwa wa maradhi ya moyo ambaye ni Mkurugenzi wa Heart team Africa Foundation, DkNaiz Majani amesema (JKCI), inahitaji shilingi bilioni 1.6 kwaajili ya kuwafanyia upasuaji wa moyo watoto 420 wanaougua maradhi ya moyo ambao wazazi wao hawana uwezo wa kugharamia matibabu yao.

Amesema HTFA kwa kushirikiana na JKCI mwaka jana walifanya harambee kukusanya fedha za matibabu kwa wagonjwa wa moyo ambapo GGM ni miongoni mwa wadau wengi waliotoa fedha kugharamia matibabu hayo.

“Tulipowaomba GGM walichangia shilingi milioni 56, matibabu ya moyo ni gharama kubwa sana duniani kote na kwa hapa Tanzania asilimia 70 ya matibabu hayo gharama inakuwa kwa serikali na asilimia 30 kwa wazazi lakini bado asilimia 30 ni kubwa sana kwa mtanzania wa kawaida,” alisema

Alisema kwa mwaka 2025 HTAF ilifanikiwa kusaidia watoto 303 kupata matibabu ya moyo kwa upasuaji wa moyo na asilimia tano wamesaidiwa na GGM na maendeleo yao ni mazuri kwa kiwango cha asilimia 95.

Alisema watoto waliosaidiwa na kufanyiwa upasuaji kupitia fedha zilizotolewa na GGM wametoka mikoa 11 ya Dar es Salaam, Kilimanjaro, Iringa, Lindi, Kibosho, Mbeya, Singida, Handeni, Pwani na Mbeya.

Dk Naiz alisema katika kila watoto 100 wanaozaliwa wakiwa hai mmoja au wawili wanakuwa na tatizo la moyo na kuongeza kuwa takwimu za hapa nchini ni kwamba kila mwaka wanazaliwa watoto milioni mbili kwa hiyo kuna watoto 10,000 ambao kila mwaka wanazaliwa na matatizo ya moyo.

Makamu wa Rais wa GGM, Simon Shayo, alisema wanaona fahari kuwa sehemu ya jitihada za kusaidia kuokoa maisha ya watoto wanaougua moyo na alitoa wito kwa taasisi mbalimbali kuunga mkono jitihada zinazofanywa na JKCI kuokoa maisha ya watoto wanaougua moyo.

“GGM tunajisikia fahari kubwa sana kuwa sehemu ya juhudi hizi, hatujutii na tunaona ni wajibu wetu kuwasaidia watanzania katika sekta hii ya afya, napenda kuwaambia watu wa sekta binafsi kuwa biashara unayofanya itakuwa na faida tu pale itakapokuwa inasaidia kubadilisha ustawi wa watu,” alisema

“Hapa JKCI kuna kazi ya kuwaokoa watoto na kurejesha tabasamu kwao, sisi GGM tunaahidi kuendelea kushirikiana na JKCI, ingawa hatujapata maombi rasmi lakini naamini mkileta ombi tutaweka kwenye mpango wetu wa utekelezaji,” alisema

Mkurugenzi Mkuu wa Global Medicare, Abdulmalik Mollel aliishukuru GGM kwa namna ambavyo imekuwa mstari wa mbele kusaidia watoto wanaougua moyo kutibiwa katika taasisi ya JKCI.

RELATED ARTICLES

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisment -
NMB Tanzania

Most Popular

Recent Comments