
WAKALA wa kiungo wa kati wa Barcelona, Dani Olmo, amethibitisha kuwa timu hiyo ya Hispania ilikataa ofa iliyoweka rekodi ya dunia kutoka kwa Paris Saint-Germain kwa ajili ya winga, Lamine Yamal.
Iliripotiwa mapema msimu wa majira ya joto kuwa PSG, katika kutafuta mbadala wa Kylian Mbappe, walipendekeza dili la thamani ya euro milioni 250 ili kumsajili winga huyo siku chache kabla ya siku yake ya kuzaliwa ya kutimiza umri wa miaka 17.
Sakata hilo liliisha ghafla kama lilivyoanza, huku Barcelona wakiripotiwa kurudisha ofa hiyo haraka sana, huku mashabiki wengi wakihoji iwapo dau la PSG lipo kweli.
“Jambo moja ninalojua kwa uhakika ni kwamba Barcelona walikataa ofa kubwa kwa Lamine Yamal kutoka PSG miezi kadhaa iliyopita,” alisema wakala Andy Bara akiiambia Podcast Inkubator.
“Mkataba huo ulikuwa na thamani ya karibu euro milioni 250.”
Bara, ambaye pia anawakilisha wachezaji kama Nacho Fernandez na Mikayil Faye, aliendelea kujadili uhamisho wa Olmo kwenda Barcelona msimu huu wa majira ya joto.
Barcelona ililazimika kufanya kazi kwa bidii kutafuta fedha za kumsajili Olmo, ambaye alilazimika kusubiri wiki mbili kabla ya klabu hiyo kumudu kumsajili kwenye kikosi chao cha LaLiga, lakini Bara alisisitiza Olmo hakuwahi kuwa na mashaka yoyote juu ya kufanya mabadiliko hayo.
“Vyombo vya habari vilipiga kelele nyingi, lakini Rais Joan Laporta aliniambia nisiwe na wasiwasi na kwamba baada ya siku 15 itasuluhishwa kama ilivyotokea,” Bara alieleza.