Benki ya TCB yaahidi kuongezakasi uwekezaji soko la Kimataifa

BENKI ya Biashara Tanzania (TCB) imeendelea kuthibitisha dhamira yake ya kupanua wigo wa uwekezaji nje ya mipaka ya nchi.

Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya TCB, Adam Mihayo, ameyasema hayo jana wakati akizungumza kwenye kikao kazi cha siku tatu kilichofunguliwa na Rais Samia Suluhu Hassan na kuwakutanisha wenyeviti wa bodi na watendaji wakuu wa taasisi za umma kujadiliana mikakati mbalimbali ya mageuzi ndani ya taasisi za umma na uwekezaji wenye tija.

Kauli mbiu ya kikao kazi hicho ni “Mikakati ya Taasisi na Mashirika ya Umma Nje yaTanzania” ambaho inagusia namna ambavyo taasisi na mashirika ya umma yanaweza kupanua wigo nje ya soko la ndani.

Mihayo amesema ili kufanikiwa nje ya mipaka ya Tanzania ni lazima soko lengwa walitambue kwa kufanya tafiti za kina ili kubaini mianya ya fursa na kutengeneza bidhaa na hudumakadri ya mahitaji ya soko la kimataifa.

Amesisitiza pia umuhimu wa mashirika hayo kuunda ubia wa kimkakati, ushirikiano na muungano ili kutumia mtandao wao wa ndani na utaalamu.

“Muundo wetu wa kibiashara unatakiwa uwe wa kibunifu na wenye uwezo wa kubadilika kuendana na mazingira ili kukabiliana na mahitaji tofauti tofauti ambayo ni muhimu ili kufanikiwa katika soko la kimataifa,” amesema.

Mihayo ameendelea kufafanua kuhusu umuhimu wa ushirikiano baina ya taasisi za umma.

“Ni muhimu kutumia uwezo wa mashirika yetu kufanya kazi tukiungana pamoja kwa kushirikishana takwimu, kupanga mikakati pamoja na kusadiana katika utoaji wa huduma. Kwa kufanya hivyo, tutaboresha rasilimali zetu na pia tutawapa wateja wetu huduma bora kulingana na mahitaji yao na kujenga imani yao kwetu,” alisema.

Akielezea utekelezaji uliofanywa na benki hiyo, Mihayo ametaja mafanikio ya hivi karibuni ikiwamo uzinduzi nchini Comoro wa huduma za kibenki kwa Watanzania waishio nje ya nchi (Diaspora Banking).

“Hii inaonyesha dhamira yetu ya kutoa huduma za kibenki nje ya mipaka na kuyafikia mahitaji ya Watanzania wote dunia nzima. Katika dhamira hii, tunatarajia kuwa katika miaka miwili ijayo tutaipeleka TCB katika Soko la Hisa (Dar es Salaam Stock Exchange), hivyo kumpa kila Mtanzania fursa ya kumiliki hisa na kuwa sehemu ya mafanikio ya taasisi hii,” alisema.

Akihitimisha hotuba yake, Mihayo ametoa wito kwa taasisi na mashirika ya umma kutobweteka na soko la ndani, bali kuiga mfano wa mataifa yaliyofanikiwa kujipenyeza nchini mwetu na kuanzisha biashara zinazostawi.

Leave a Comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *