Kocha Azam ajitetea sare na Pamba Ligi Kuu

Kocha mpya wa Azam FC, Rachid Taoussi, raia wa Morocco, amesema umaliziaji mbaya na kuchelewa kwa baadhi ya wachezaji waliokwenda kuzichezea timu zao za taifa katika michezo ya kufuzu fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON), ndiko kulikosababisha kutoka suluhu juzi dhidi ya Pamba Jiji FC.

Akizungumza baada ya kumalizika kwa mchezo huo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, uliopigwa Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam, kocha huyo alisema bado ana muda mfupi kwenye kikosi hicho na kwamba bado anakiandaa ili kicheze kwa jinsi anavyotaka yeye.

“Tulikuwa tunataka kushinda, lakini si rahisi, kwa siku tano bado tunafundisha jinsi ya kushambulia na kumalizika nafasi, nimefurahi kipindi cha kwanza tumefanya vizuri sana, tumeshambulia kama nilivyokuwa nataka, tatizo letu lilikuwa kwenye kumalizia.

Kingine ni kwamba wachezaji wetu walichelewa kujiunga kutoka kwenye vikosi vya timu ya taifa, kwa muda wa siku kadhaa hawakuwa kwenye mikono yangu, hii nayo imeathiri sana mipango yangu kwenye mchezo wa leo,” alisema Taoussi.

Ilikuwa ni mechi ya kwanza ya Ligi Kuu Bara kwa kocha huyo ambaye ameichukua timu kutoka kwenye mikono ya Msenegal Youssouph Dabo, aliyeoneshwa mlango wa kutokea baada ya kikosi hicho kusukumizwa nje ya Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya awali dhidi ya APR, pamoja na kutoka suluhu katika mchezo wa kwanza wa Ligi Kuu dhidi ya JKT Tanzania.

 Naye Kocha wa Pamba Jiji, Goran Copunovic, ameeleza kufurahishwa na jinsi vijana wake walivyopambana, hasa kipindi cha pili.

“Tumecheza vema, hasa kipindi cha pili, tumewashambulia sana wapinzani wetu, timu yetu ndiyo kwanza imepanda daraja, tulikuwa tunacheza na timu kubwa, yenye uzoefu kwenye Ligi Kuu, iliyotoka pia kucheza mechi za kimataifa, tulistahili ushindi au sare tuliyoipata,” alisema kocha huyo raia wa Serbia.

Matokeo ya mechi ya juzi, yameifanya Pamba Jiji kushika nafasi ya nane kwenye msimano ikiwa na pointi tatu na michezo mitatu, Azam ikiwa ya 10, ambapo ina pointi mbili na mabao mawili mpaka sasa.

Leave a Comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *