
Waokoaji katika eneo la mashariki mwa Urusi Urusi hawakupata mtu yeyote aliyenusurika kwenye mabaki ya helikopta iliyotoweka ikiwa imebeba watu 22 wengi wao wakiwa watalii.
Ndege hiyo ilitoweka siku ya Jumamosi baada ya kupaa kutoka kambi moja karibu na volcano ya Vachkazhets katika rasi ya Kamchatka.
Maafisa wanasema miili 17 ilikuwa imepatikana kufikia sasa.
Eneo hilo, ambalo ni kivutio maarufu cha watalii, ni maarufu kwa volkano zake .
Chanzo cha ajali hiyo hakijafahamika.
Ajali kama hizo hutokea mara kwa mara katika eneo la mashariki mwa Urusi, ambalo lina watu wachache na linakabiliwa na hali mbaya ya hewa.
Miaka mitatu iliyopita watu wanane waliuawa wakati helikopta ya watalii ilipoanguka katika ziwa huko Kamchatka.
Helikopta ya Mi-8T iliyotoweka kwenye rada siku ya Jumamosi ilikuwa na watalii 19 na wafanyakazi watatu.

Mabaki hayo yalipatikana Jumapili asubuhi katika eneo lenye milima, Gavana wa Kamchatka Vladimir Solodov alisema kwenye Telegram.
Picha zilizochapishwa kwa programu ya ujumbe na wizara ya dharura ya Urusi zilionyesha vifusi vya helikopta vikiwa karibu na mteremko karibu na kilima kikubwa chenye miti.
Maafisa walisema mabaki hayo yalipatikana karibu na eneo ambapo helikopta hiyo ilipotea katika rada.
Afisa wa wizara ya dharura, Ivan Lemikhov, anasema miili 17 imepatikana hadi sasa na utafutaji wa wale ambao bado hawajapatikana umesitishwa, na unaotarajiwa kuendelea alfajiri siku ya Jumatatu.
Shirika la habari la Interfax la Urusi liliripoti kwamba hitilafu, huenda ilisababishwa na ukungu.
Awali, maafisa walisema kuwa ukungu mzito ulikuwa unatatiza juhudi za waokoaji.
Ndege hiyo ilimilikiwa na Vityaz-Aero, kampuni ya Kamchatka ambayo hupanga safari za watalii.
Ikiwa imeundwa wakati wa enzi ya Soviet, helikopta hiyo ya Mi-8 bado inatumika sana nchini Urusi.
