
MAMLAKA ya Usimamizi wa Bandari nchini (TPA), imesema shehena ya makasha imeongezeka kutoka 7,151 mwezi Aprili 2024 hadi kufikia makasha 20,151 kufikia mwezi Julai 2024.
Ongezeko hilo linaelezwa kusababishwa na uwekezaji uliofanywa na DP World katika bandari ya Dar es Salaam wenye thamani ya takriban dola milioni 250 kwa ajili ya uendeshaji wa magati 0-7 bandarini.
Hayo yalisemwa jana na Meneja wa shughuli na uratibu wa TPA, Josephat Lukindo, wakati akiwasilisha ripoti fupi ya utendaji wa bandari hiyo kwa Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Amos Makala, wakati wa ziara yake badarini jana.
Alisema pesa hizo zimetumika kuboresha utendaji wa bandari hiyo katika maeneo matatu baada ya kukabidhiwa na mamlaka ya bandari Aprili mwaka huu.
“Kwa uzoefu tulionao wa uendeshaji wa bandari, tuliamua kuanza na uboreshaji wa maeneo matatu muhimu ili kuongeza ufanisi zaidi,†alisema Lukindo.
Alisema sehemu ya kwanza kampuni ya DP World kupitia kampuni tanzu ya DP World Dar es Salaam iliyoanzishwa kusimamia bandari hiyo ilifanya manunuzi ya mitambo ya kisasa.
Alisema ilifanya ukarabati wa mitambo mibovu iliyokuwa ikitumika bandarini hapo na kufanya manunuzi ya vifaa vipya yakiwemo matrekta 20 ya kubebea mizigo pamoja na matela 31, jenerela saba zenye ukubwa wa KV 10,000 kila moja kwa ajili ya kuendeshea mitambo umeme unapokatika na vifaa vya kubebea mizigo mizito (cranes) .

“DP World ilifanya usimikaji wa mifumo ya kisasa ya TEHAMA kwa ajili ya utendeshaji wa bandari hiyo kwasababu awali tulikuta mifumo ambayo imepitwa na wakati na kuamua kuweka mifumo ya kisasa kuendana na maendeleo ya teknolojia,†alisema.
Alisema uwekezaji huo wa mifumo ya kisasa umesababisha manufaa makubwa ndani ya kipindi cha miezi mitatu iliyochangia ongezeko la shehena ya makasha ikiwa sawa na ongezeko la asilimia 18.2.
“Uwekezaji huu utaifanya Bandari ya Dar es Salaam kuwa katika ushindani na bandari nyingine kubwa barani Afrika ikiwemo ya Morocco,†alisema
Akizungumza bandarini hapo, Makalla alipongeza utendaji kazi wa TPA na kufurahishwa na mafanikio hayo akielezea kuwa ni kielelezo tosha kwa wale waliokuwa wanaubeza uwekezaji huo.
“Kuna watu wao kazi yao ni kupinga kila kitu hata wakati Serikali inanunua ndege walipinga pia na cha ajabu wanafurahia kupanda ndege hizo hivi sasa,†alisema Makala na kuongeza kuwa wengine walipinga uwekezaji wa treni ya SGR na hata ujenzi wa bwawa la Mwalimu Nyerere kwa ajili ya kuzalisha umeme.
Alisema CCM inaiunga mkono Serikali kwa uwekezaji huo katika maeneo yote muhimu ikiwemo bandari kwani hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa ilani ya CCM.
“Tupo katika ziara ya kutembelea miradi mbalimbali ya uwekezaji iliyotekelezwa na serikali ukiwemo wa Bandari ya Dar es Salaam na kiukweli tumefurahishwa sana na maendeleo tuliyaona,†alisema.
Naibu Mkurugenzi wa TPA, Juma Kijavara alisema mafanikio yaliyopatikana ndani ya kipindi kifupi cha uwekezaji wa DP World yametokana na hatua mbalimbali zilizochukua ili kuongeza ufanisi wa utendaji na kuvutia wafanyabiashara zaidi wa ndani na nje ya nchi.
“Bandari ya Dar es Salaam itakuwa na uwezo wa kushindana na bandari nyingine duniani kwa kutoa huduma bora na kwa haraka kutokana na uwekezaji mkubwa uliofanyika,†amesema Kijavara.
