Sunday, November 2, 2025
spot_img
HomeBiasharaMNRT SACCOS yatoa mikopo ya zaidi ya Bilioni 1.2 kwa wanachama wake

MNRT SACCOS yatoa mikopo ya zaidi ya Bilioni 1.2 kwa wanachama wake

Chama cha Ushirika wa Akiba na Mikopo cha MNRT SACCOS LTD kimefanikiwa kutoa mikopo yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 1.2 kwa wanachama wake katika kipindi cha mwaka mmoja, hatua inayolenga kuwawezesha kujikwamua kiuchumi na kuboresha ustawi wao.

Hayo yamesemwa leo Oktoba 25, 2025, na Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, ambaye pia ni Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu, Bernard Marcelline, wakati akifungua mkutano mkuu wa tano wa MNRT SACCOS LTD uliofanyika katika ukumbi wa TANAPA, jijini Dodoma.

Marcelline amesema kuwa chama hicho, ambacho kwa sasa kina zaidi ya wanachama 700, kimechangia kuongeza tija na ufanisi kazini kwa kuwafanya watumishi kuwa na utulivu kutokana na uhakika wa kipato kupitia huduma za kifedha wanazopata.

“Kutoa mikopo ya zaidi ya bilioni 1.2 kwa mwaka maana yake ni fedha zimeingia kwa wanachama na zimekwenda kufanya shughuli za kiuchumi za maendeleo katika sehemu wanazoishi,” amesema Marcelline.

Aidha, amewahimiza watumishi wa Wizara ya Maliasili na Utalii ambao bado hawajajiunga na chama hicho kufanya hivyo haraka, akieleza kuwa MNRT SACCOS inakua kwa kasi kubwa na kutoa manufaa halisi kwa wanachama wake.

Ameongeza kuwa wanachama wanaokopa wanapaswa kutumia mikopo hiyo kwa malengo yaliyokusudiwa na kurejesha kwa wakati, ili kujenga uaminifu na kuhakikisha upatikanaji endelevu wa huduma kwa wengine.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa MNRT SACCOS LTD, Wilfred Msemo, amesema chama hicho kimeendelea kukua kwa kasi, ambapo mwaka huu kimefanikiwa kutoa gawio la shilingi milioni 76 kwa wanachama wake, kuchangia katika shughuli za kijamii, na kuongeza wanachama wapya 138.

Msemo ameongeza kuwa mafanikio hayo yanatokana na ushirikiano mzuri uliopo kati ya wanachama, viongozi wa chama, na Wizara mama, huku akisisitiza dhamira ya kuendelea kuimarisha huduma na kupanua wigo wa mikopo ili kufikia wanachama wengi zaidi.

RELATED ARTICLES

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisment -
NMB Tanzania

Most Popular

Recent Comments