Vijana kutoka maeneo mbalimbali nchini wamekutana jijini Mwanza kwa lengo la kuwahamasisha wenzao kujitokeza kwa wingi katika uchaguzi mkuu ujao, wakisisitiza umuhimu wa kutumia kura kama chombo cha mabadiliko chanya na kulinda amani ya taifa.
Kongamano hilo lililowakutanisha vijana kutoka mikoa tofauti nchini limeangazia nafasi ya vijana katika mchakato wa uchaguzi na umuhimu wa kudumisha amani, utulivu na mshikamano wa kitaifa, mambo yaliyotajwa kuwa nguzo kuu ya maendeleo ya Tanzania.
Washiriki wa kongamano hilo walisema kuwa vijana wanayo nafasi ya kipekee katika kuamua hatima ya taifa kupitia kura zao, wakihimiza wenzao wajitokeze kwa wingi siku ya kupiga kura ifikapo Oktoba 29, 2025.


Mmoja wa washiriki, Pendo Msote, alisema vijana ndio nguzo kuu ya taifa na hivyo wanapaswa kutumia nafasi yao ipasavyo.
“Sisi vijana tunayo nafasi kubwa ya kubadili hatima ya nchi yetu kwa kuchagua viongozi bora. Hatutaki kuona amani yetu inavunjwa, hivyo ni muhimu tushiriki kwa wingi katika uchaguzi,” alisema Msote.


Kwa upande wake, Kashinje John alisisitiza kuwa kura ni sauti ya kila kijana na ni nyenzo muhimu ya kuleta mabadiliko ya kweli katika taifa.
“Kura yako ni sauti yako. Ni njia ya kuwakilisha wale ambao hawana fursa ya kupiga kura. Kura moja inaweza kuamua mustakabali wa taifa letu,” alisema Kashinje.
Aidha, alikumbusha umuhimu wa kulinda amani kabla, wakati na baada ya uchaguzi.
“Amani ni urithi wetu. Tunaweza kuichukulia kama kitu cha kawaida, lakini ni hazina kubwa isiyopaswa kuchezewa,” aliongeza.
Kwa mujibu wa Ibara ya 74 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Tume Huru ya Uchaguzi imepewa jukumu la kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa uhuru, haki na amani. Kura imeelezwa kuwa si tu haki bali pia ni wajibu wa kila Mtanzania, hususan vijana, kuchangia katika ujenzi wa taifa bora.
Naye aliyewahi kuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, alisema kuwa uchaguzi ni tukio la kihistoria linalodhihirisha dhamira ya Watanzania katika kudumisha demokrasia na utulivu wa nchi.
“Siku ya kupiga kura ni siku takatifu — ni siku ambayo Tanzania hujionyesha kwa mataifa mengine kama taifa lenye demokrasia, utulivu na amani,” alisema Nyalandu.
Aliongeza kuwa Tanzania imeendelea kuwa mfano wa kuigwa katika ukanda wa Afrika kutokana na amani na utulivu wake wa kipekee.
“Hii ni amani ya thamani kubwa ambayo tunapaswa kuilinda kwa gharama yoyote,” alihitimisha.
Katika hitimisho la kongamano hilo, vijana waliahidi kuendelea kuhamasishana kuhusu umuhimu wa kushiriki kwenye uchaguzi, wakisisitiza kuwa kufanya hivyo ni kutekeleza wajibu wao wa kiraia na kuchangia katika kuimarisha misingi ya kidemokrasia nchini.





