Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS), Profesa Appolinary Kamuhabwa, amesema chuo hicho kimeendelea kuimarisha mshikamano wa wahitimu wake kwa kuwaunganisha kupitia shughuli za michezo, matembezi na mbio za marathon zinazofanyika mara moja kila mwaka.
Profesa Kamuhabwa amesema lengo la mpango huo ni kuwakutanisha wahitimu waliomaliza masomo yao katika miaka mbalimbali na wanaoendelea kufanya kazi sehemu tofauti, ili warejee chuoni kama “nyumbani” na kushiriki mawazo kuhusu maendeleo ya MUHAS na mchango wanaoweza kuutoa.
Amesema MUHAS pia imeanzisha mfumo wa kidijitali unaowaunganisha wahitimu kupitia majukwaa mbalimbali ya mtandaoni, ikiwemo tovuti na makundi ya WhatsApp kulingana na fani au mwaka wa kuhitimu, hatua inayowezesha mawasiliano na ushirikiano wa karibu zaidi.
“Kwa mara ya nne sasa tunafanya tukio hili na mwitikio umekuwa mkubwa. Mwaka huu zaidi ya wahitimu 500 wamejisajili kushiriki. Hii inatusaidia kupanga mikakati mbalimbali ya kuendeleza chuo,” amesema Profesa Kamuhabwa.
Katika hatua nyingine, amesema MUHAS imeanzisha mfuko wa hisani uitwao Ali Hassan Mwinyi MUHAS Endowment Trust Fund, kwa lengo la kuenzi mchango wa Mkuu wa kwanza wa chuo hicho, Hayati Ali Hassan Mwinyi, na kuwezesha maendeleo ya taasisi hiyo, ikiwemo ujenzi wa mabweni, kuimarisha miundombinu na kusaidia wanafunzi.
Ameeleza kuwa chuo hicho kimeendelea kuvutia wanafunzi wa kigeni kutoka mataifa mbalimbali ikiwemo Marekani, Ujerumani, Australia na Sweden, wengi wao wakija kwa mafunzo ya muda mfupi baada ya kujifunza sifa za MUHAS kupitia tovuti na mitandao ya kijamii ya chuo.
Kwa sasa, wanafunzi wa kigeni wanachangia takribani asilimia 10 ya udahili wote, huku lengo likiwa ni kufikia kati ya asilimia 15 hadi 30 kwa miaka ijayo, sambamba na upanuzi wa miundombinu na kuongezeka kwa idadi ya watumishi kutokana na vibali vipya vya ajira vilivyotolewa na Serikali.
Profesa Kamuhabwa pia amesisitiza umuhimu wa mazoezi ya mwili kama njia ya kuzuia magonjwa yasiyoambukiza kama kisukari na shinikizo la damu, akisema MUHAS kama chuo cha afya kina wajibu wa kutoa mfano kwa jamii.
Akizungumza kwa niaba ya waandaaji, Mhadhiri Mwandamizi wa Afya ya Jamii na Mkuu wa Kitengo cha Umataifaifishaji na Convocation MUHAS, Mariam Amour, amesema tukio hilo lijulikanalo kama MUHAS Fun Run Season 4 limefanyika kwa mwaka wa nne mfululizo na linaendelea kukua kila mwaka.
Amesema mwaka huu zaidi ya watu 500 wameshiriki, tofauti na mwaka wa kwanza ambapo walikuwa takribani 200, huku fedha zilizokusanywa zikielekezwa katika mfuko wa Ali Hassan Mwinyi MUHAS Trust Fund kwa ajili ya kusaidia shughuli za ufundishaji, tafiti, miundombinu na ufadhili wa wanafunzi.
Naye Rais wa Jumuiya ya Wahitimu wa MUHAS, Marsha Macatta Yambi, amesema tukio hilo limevuka malengo yaliyowekwa baada ya idadi ya washiriki kuwa kubwa kuliko ilivyotarajiwa, jambo linaloonesha mshikamano na moyo wa uzalendo miongoni mwa wahitimu.
Amesema kupitia mfuko huo wa hisani, chuo kinatarajia kuendelea kuwekeza katika maendeleo ya taaluma, utafiti, mazingira ya wanafunzi pamoja na ustawi wa afya kwa ujumla, huku akitoa wito kwa wahitimu wengine kujiunga na kushiriki kikamilifu katika shughuli za chuo.





