Wednesday, March 25, 2026
spot_img
HomeHabariNguvu ya miamala ya simu katika uchumi wa Tanzania

Nguvu ya miamala ya simu katika uchumi wa Tanzania

Na Mwandishi Wetu

Mara nyingi mijadala ya maendeleo ya uchumi huzungumzia miradi mikubwa inayoweza kuonekana kwa macho kama barabara, reli, bandari, viwanja vya ndege au miradi ya nishati, pengi ni kwakuwa inahusisha uwekezaji mkubwa na kugusa sekta nyingi za uchumi.

Hata hivyo, mbali na miradi hiyo mikubwa, kuna nguvu nyingine ya miundombinu ambayo haijengwi kwa saruji wala chuma na haihitaji mitambo mikubwa ya ujenzi, bali ipo katika simu za mkononi zinazotumiwa na mamilioni ya watu kila siku.

Mkurugenzi wa M-Pesa Tanzania, Epimack Mbeteni, anasema nguvu hiyo inatokana na maendeleo ya huduma za fedha kwa njia ya simu  ambazo zimebadilisha namna watu wanavyofanya miamala na kushiriki katika shughuli za uchumi.

“Kuna nguvu zinazochochea uchumi kwa sauti kubwa kama miradi mikubwa ya miundombinu au mageuzi ya sera. Lakini pia kuna nguvu zinazofanya kazi kimya kimya, zikiwa zimejikita katika maisha ya kila siku ya wananchi na athari zake ni kubwa katika mabadiliko ya uchumi,” anasema Mbeteni.

Kwa mujibu wa Mbeteni, huduma za fedha kwa simu zimekuwa sehemu muhimu ya uchumi wa Tanzania kwa sababu zinawapa wananchi wengi zaidi fursa ya kushiriki katika mfumo wa kifedha bila kujali wanapoishi au kiwango cha kipato walicho nacho.

Anasema huduma za fedha kwa simu zilipoanza kutumika nchini mwaka 2008, zilionekana zaidi kama njia mbadala ya kutuma au kupokea fedha kwa haraka. Wakati huo, wananchi wengi walizitumia kama mbadala wa kubeba fedha taslimu au kutuma pesa kwa ndugu walioko mbali.

“Huduma hizi zilipoanza, zilionekana kama urahisi tu wa kutuma na kupokea pesa tu. Wachache walitarajia kwamba zingekuja kuwa sehemu muhimu ya shughuli za kila siku za uchumi,” anasema.

Takwimu za Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) za Desemba 2025 zinaonyesha kuwa Tanzania ilikuwa na zaidi ya akaunti milioni 76.5 za huduma za fedha kwa simu katika mitandao mbalimbali.

Kati ya akaunti hizo, asilimia 41.2 ni watumiaji wa M-Pesa, hali inayoonyesha ushindani mkubwa uliopo katika soko la huduma za fedha kwa simu nchini lakini pia uongozi wa M-Pesa sokoni.

“Leo hii zaidi ya Watanzania milioni 31 wanatumia M-Pesa kikamilifu, wakihamisha mabilioni ya shilingi kidijitali kila mwezi kwa usalama na ufanisi,” anasema Mbeteni na kuongeza kuwa ukuaji wa huduma za M-Pesa umetokana kwa kiasi kikubwa na uaminifu wa watumiaji pamoja na uthabiti wa mfumo wake wa miamala.

Kadhalika Mbeteni anasema, huduma ya kurejesha muamala (Self-Reversal) imewasaidia watumiaji kurekebisha miamala iliyofanywa kimakosa moja kwa moja kupitia simu zao.

Huduma zaidi na M-Pesa

Mbeteni anasema kama ambavyo miundombinu mingine huchochea na kurahisisha biasharakwa, kupunguza gharama na kufungua fursa za biashara za kikanda, M-Pesa nayo kwa namna yake inafanya hivyo, inaweka urahisi wa miamala yote ya kibiashara na huduma za kifedha kwa ujumla wake.

Kama ambavyo bandari zinaunganisha Tanzania na biashara ya kimataifa, M-Pesa inaunganisha wasio na akaunti za benki na biashara rasmi na wakati gridi za umeme zikiwezesha uzalishaji viwandani, M-Pesa huwezesha ukwasi na mtiririko wa mtaji wa kazi kwa biashara ndogo na za kati

Kwa upande wa biashara, jukwaa la M-Pesa Business limewasaidia wafanyabiashara kupokea malipo kwa njia ya kidijitali na kusimamia fedha zao kwa ufanisi zaidi.

Kupitia M-Wekeza, watumiaji wanaweza kuwekeza kiasi kidogo cha fedha na kupata faida. M-Koba inasaidia vikundi vya kijamii kuweka akiba kwa pamoja, huku Songesha ikitoa mikopo midogo ya muda mfupi kwa watumiaji wanaokabiliwa na changamoto za kifedha za muda.

Kwa wale wanaofanya miamala ya kimataifa au malipo ya mtandaoni, M-Pesa Visa Virtual Card imefungua fursa mpya za kufanya malipo nje ya mipaka ya nchi.

Mbali na huduma za kifedha, M-Pesa pia imeunganishwa na huduma nyingine muhimu zinazogusa maisha ya wananchi, kupitia VodaBima, watumiaji wanaweza kupata huduma za bima ikiwemo bima ya magari.

Aidha, mfumo wa M-Pesa umeunganishwa na mfumo wa malipo ya Serikali, unaowawezesha wananchi kulipia huduma mbalimbali za serikali moja kwa moja kupitia simu zao.

“Huduma hizo ni zile zote ambazo taasisi za Serikali hutoa ‘control number’ ambazo ni pamoja na malipo ya pasi za kusafiria, kodi ya ardhi na faini mbalimbali za serikali.

Upande mwingine, M-Pesa imechangia kuunda ajira na fursa za kipato kwa maelfu ya watu nchini. Kwa mujibu wa Mbeteni, huduma hiyo inahusisha zaidi ya mawakala 200,000 na wafanyabiashara zaidi ya 600,000 wanaotumia mfumo huo katika shughuli zao za kila siku.

Hivi sasa thamani ya miamala inayofanyika kupitia mfumo huo kila mwezi inazidi Sh16 trilioni. Kila Shilingi inayopita M-Pesa huzunguka kwa haraka zaidi, hufika kwa watu wengi zaidi na huchochea shughuli nyingi zaidi za kiuchumi kuliko fedha taslimu.

Mzunguko wa fedha kidijitali ni nyenzo muhimu katika mzunguko wa ukwasi miongoni mwa Watanzania sawa na damu inavyosambaa mwilini, Mbeteni anasema huduma za fedha kwa simu zinapaswa kuonekana kama aina mpya ya miundombinu inayochochea uchumi wa kisasa.

“Katika nchi ambayo mara nyingi maendeleo hupimwa kwa miradi mikubwa ya miundombinu, huduma za fedha kwa simu zinawakilisha aina nyingine ya miundombinu ya kidijitali ambayo inapatikana kwa watu wengi na kusambaa kila mahali,” anasema.

Mbeteni anasema, mchango wa miamala ya simu unaweza usionekane moja kwa moja kama daraja au reli mpya, lakini athari zake zinaonekana katika uimara wa biashara ndogo, kuongezeka kwa shughuli za kifedha na kuimarika kwa ushiriki wa wananchi katika uchumi.

RELATED ARTICLES

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisment -
NMB Tanzania

Most Popular

Recent Comments