Dar es Salaam, 6 Mei 2025 — Rais wa Jumuiya ya Wanafunzi wa Taasisi za Elimu ya Juu nchini (TAHLISO), Geofrey Kiliba, amefanya ziara rasmi katika Ofisi za Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (NACTVET) kwa lengo la kuwasilisha changamoto mbalimbali zinazowakabili wanafunzi wa vyuo vya kati na vyuo vya ufundi nchini.
Ziara hiyo ameifanya leo kufuatia kukamilika kwa mfululizo wa ziara alizozifanya katika mikoa mbalimbali, ambako alipata nafasi ya kusikiliza na kukusanya maoni na changamoto kutoka kwa wanafunzi katika taasisi mbalimbali za elimu ya juu.
Katika ziara hiyo, Rais Kiliba alipokelewa na Katibu Mtendaji wa NACTVET, Dk. Mwajuma, pamoja na ujumbe wake wa viongozi waandamizi wa Baraza hilo. Mazungumzo yao yalilenga kuimarisha ushirikiano baina ya TAHLISO na NACTVET katika kushughulikia masuala ya msingi yanayowahusu wanafunzi, hususan yanayohusiana na ajira baada ya kuhitimu, ubora wa mafunzo kwa vitendo, usimamizi wa mitaala, na uboreshaji wa mazingira ya kujifunzia.
Rais Kiliba amesisitiza dhamira ya TAHLISO katika kuendeleza ushirikiano na taasisi za Serikali ili kuhakikisha kuwa sauti ya mwanafunzi inasikika na changamoto zake kutatuliwa kwa wakati. Aidha, Dk. Mwajuma amepongeza juhudi hizo na kuahidi kuwa Baraza litaendelea kushirikiana kwa karibu na TAHLISO katika kuhakikisha elimu ya ufundi nchini inakuwa chachu ya maendeleo ya Tanzania.




