Singida BS yajifungia Dar

KIKOSI cha Singida Black Stars kimeweka kambi jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kufanya mazoezi kwenye viwanja vya nyasi bandia kabla ya kuivaa Kagera Sugar, Jumamosi ijayo kwenye Uwanja wa Kaitaba ulioko Bukoba, mkoani Kagera.

Ofisa Habari wa Kagera Sugar, Hussein Massanza, amesema jana wamewasili Dar kwa lengo la kuweka mikakakati ya kuhakikisha wanapata pointi tatu muhimu za mchezo huo.

“Tumekuja KMC kufanya mazoezi kwa sababu tunakwenda kucheza dhidi ya Kagera Sugar ambako kuna uwanja wa nyasi bandia. Singida hakuna kiwanja chenye nyasi bandia, Uwanja wa Kaitaba una kapeti, tupo hapa kwenye Uwanja wa KMC, ambao ni wa nyasi bandia, moja wa viwanja bora, na bado ni mpya, ” alisema Massanza.

Naye Kocha Msaidizi wa timu hiyo, Denis Kitambi, alisema wanafanya maandalizi ‘kabambe’ kwa sababu wanataka ushindi na si matokeo mengine tofauti.

Kitambi alisema malengo ya timu hiyo ni kumaliza katika nafasi nne za juu msimu huu wa 2024/2025.

“Nia yetu msimu huu ipo wazi, tunataka kumaliza katika nafasi nne za juu, unajua kila baada ya mchezo tunafanya tathmini, ndiyo tumeshinda mabao 3-1 mchezo uliopita, lakini kuna maeneo tumeyaona yana mapungufu tunahitaji kuboresha, na moja ambalo tunataka kulifanya ni kutoruhusu mabao mepesi,” Kitambi aliongeza.

Alisema anahitaji kukamilisha ‘biashara’ mapema ili kujiondoa kwenye ‘presha’ wakati wa lala salama.

Leave a Comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *