Tamasha la utamaduni Ruvuma kutingisha

Shamra Shamra za tamasha la utamaduni kitaifa litakalofanyika Mkoa wa Ruvuma, zinaendelea kupamba moto huku Rais Samia Sluhu Hassan akitarajiwa kuwa mgeni rasmi kwenye ufunguzi wake mwishoni mwa mwezi huu.Ufunguzi wa tamasha hilo la tatu la Mkoa wa Ruvuma unatarajiwa kufanyika tarehe 20 ya mwezi huu na litafanyika kwa muda wa siku nne mpaka tarehe 23 ambapo makabila yataonyesha tamaduni mbalimbali.

Wakazi wa Mkoa huo wameonyesha shauku kubwa ya kushiriki tamasha hilo ambalo wanalielezea kuwa litakuwa la aina yake kwani mbali na faida zingine litasaidia kuchochea shughuli za kiuchumi za mkoa huo.

Tito Mbilinyi maarufu kama Mwilamu alisema anashukuru sana kwa kuwa ugeni utakaokuja Ruvuma utasababisha manufaa makubwa ya kiuchumi kwa wananchi wa Mkoa huo.

“Hili tamasha sisi wafanyabiashara litatupa manufaa makubwa, kwenye nyumba za kulala wageni, mama lishe, mwenye teksi atanufaika ugeni ni mkubwa watu zaidi ya 5,000 si mchezo, tunawaomba viongozi wa mkoa wetu wawe wanatutengenezea fursa kama hizi,” alisema

“Rais Samia ni msikivu sana anatujali sisi watu wa sekta binafsi kwasababu zile changamoto ambazo tunakutana nazo tukimwambia huwa anazitatua haraka sana. Tunamshukuru sana na tunamkaribisha sana Ruvuma,” alisema

“Sisi ndio tunajidai kuwa tunalisha mikoa mbalimbai na mataifa mengine yenye uhaba wa chakula. Hili tamasha litatusaidia sana kuinua uchumi wetu wananchi wajitokeze kwa wingi kutumia fursa hii,” alisema

Upendo Hosia ambaye ni mdau wa hoteli mkoani humo, alisema taarifa ya ujio wa Rais Samia wamezipokea kwa furaha sana na watahakikisha wanatumia fursa hiyo kuuwezesha mkoa huo unanufaika kiuchumi.

Alisema uchumi wa Mkoa huo umekuwa ukiimarika siku hadi siku kutokana na kupita magari makubwa ya mizigo yanayochukua shehena ya mizigo kusafirisha maeneo mbalimbali.

“Nikiwa kama mama tunampokea kwa mikono miwili wanawake wa mkoa huu tumejipanga kumpokea na atafurahi kuona utamaduni wa mkoa wa Ruvuma, wafanyabiashara na wananchi nawaambia kitu kimoja kamba ujio huu ni muhimu na fursa kwasababu ugeni huo utaleta maelfu ya watu,” alisema

Tamasha hilo la tatu la utamaduni kitaifa ni tukio kubwa la kitamaduni linaloadhimishwa mkoani Ruvuma.

Lengo kuu la tamasha hili ni kuonesha na kuhifadhi urithi wa kitamaduni wa makabila mbalimbali ya Tanzania, haswa yale yanayopatikana katika mkoa wa Ruvuma.

Tamasha hilo linatoa jukwaa kwa jamii kushiriki na kuonesha muziki wa kitamaduni, ngoma, sanaa, mavazi ya kitamaduni, vyakula vya asili, pamoja na mila na desturi za jadi.Tamasha hili lina umuhimu wa kijamii, kiutamaduni na kiuchumi kwa kuwa linasaidia kuongeza hamasa ya kulinda na kuenzi urithi wa kitamaduni, huku pia likiwavutia watalii wa ndani na nje ya nchi.

Mara nyingi, washiriki kutoka mikoa mingine ya Tanzania na hata kutoka nje ya nchi hushiriki tamasha hili, na hivyo kuleta mchanganyiko wa tamaduni mbalimbali.

Mkoa wa Ruvuma ni miongoni mwa mikoa michache nchini ambayo imebarikiwa kuwa na vivutio vya aina zote za utalii,ambazo ni utalii wa ikolojia na utamaduni.

Mkoa wa Ruvuma una mapori manne ya wanyamapori ambayo ni sehemu ya mfumo wa Selous na mapori hayo ni Selous ambalo hivi sasa ni Hifadhi ya Taifa ya Nyerere lenye ukubwa wa kilometa za mraba 50,000,Pori la Liparamba lenye kilometa za mraba 571,Gesimasoa lenye kilometa za mraba 764 na Litumbandyosi lenye kilometa za mraba 464.

Hata hivyo utafiti umebaini bado kuna vivutio vingi ambavyo havijaibuliwa na kutambuliwa ili kutoa fursa za uwekezaji kwa watalii toka ndani na nje ya nchi.

Hatua mbalimbali zinachukuliwa na serikali kuanzia serikali ya awamu ya tano na sita kuhakikisha miundombinu mbalimbali inaboreshwa katika Mkoa wa Ruvuma ili kuvutia wawekezaji wa ndani na nje ya nchi.

Hivi sasa wawekezaji wameanza kuonesha nia ya kuwekeza katika Mkoa wa Ruvuma na kwamba Mkoa umeunganishwa kwa barabara za lami katika wilaya zake zote,pia usafiri wa anga na majini umeboreshwaPia serikali imetoa mwongozo wa uwekezaji wa Mkoa wa Ruvuma ambao ulizinduliwa na Waziri Mkuu Mheshimiwa Kassim Majaliwa mwaka 2019.

Mwongozo huo unapatikana kwenye tovuti ya Mkoa wa Ruvuma.

Leave a Comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *