📌 Yasema mradi huo ni ushahidi wa thamani ya kodi za wananchi katika kuchochea maendeleo ya nchi
📌Yahimiza ulipaji wa kodi kwa hiari na wakati kuwezesha utekelezaji endelevu wa miradi mingine inayoendelea nchini
Mamlaka ya Mapato nchini (TRA) imesifu matumizi sahihi ya fedha za kodi za watanzania katika Mradi wa Bwawa la Julius Nyerere kufuatia ziara yao ya kikazi Februari 14, 2026, ikieleza kuwa mradi huo unaonyesha namna kodi zinavyochochea maendeleo kwa kuongeza upatikanaji wa umeme wa uhakika nchini.
Ziara hiyo ilihusisha Viongozi na Maafisa Elimu na Mawasiliano kutoka vituo vyote nchini vya Mamlaka hiyo wakiwa na lengo la kujifunza na kujionea namna kodi za wananchi zilivyowezesha utekelezaji wa mradi huo mkubwa wa kimkakati wa taifa.
Akizungumza mara baada ya ziara hiyo, Mkurugenzi wa Elimu na Mawasiliano wa TRA, Bw. Richard Kayombo, alisema ziara yao katika Mradi wa Bwawa la Julius Nyerere ilikuwa muhimu kwa kuwa TRA ndiyo taasisi inayokusanya kodi, hivyo walitaka kujionea jinsi fedha za wananchi zinavyotumika na matokeo yake kwa maendeleo ya nchi.
Bw. Kayombo alisema mradi wa Bwawa la Julius Nyerere unaonyesha jinsi kodi zinavyobadilisha maisha ya wananchi kwa kuongeza umeme wa uhakika, kukuza biashara, uwekezaji na ukuaji wa uchumi, hivyo kuongeza wigo wa ukusanyaji wa mapato ya Serikali.
Aliongeza kuwa, ongezeko la uzalishaji wa umeme nchini linasaidia kupunguza changamoto za mgao wa umeme na kuimarisha utoaji wa huduma kwa wananchi na sekta binafsi.

“ Mradi huu unatupa ushahidi kuwa kodi za wananchi zinapotumika ipasavyo katika kuleta matokeo makubwa yanayoonekana na kugusa maisha ya jamii moja kwa moja,” alisema Bw. Kayombo.
Kwa upande wao, Maafisa Elimu na Mawasiliano wa TRA walieleza kuwa, ziara hiyo imewapa uelewa mpana kuhusu uwekezaji uliofanywa na Serikali katika sekta ya nishati na kuahidi kuwa mabalozi wazuri wa kuhamasisha ulipaji wa kodi kwa hiari na wakati.
Aidha, wameahidi kuendelea kuwaelimisha wananchi kuwa kodi wanazolipa zina mchango mkubwa katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo mfano , Bwawa la Julius Nyerere, ambalo sasa ni moja ya vyanzo muhimu vya umeme katika Gridi ya Taifa likichangia takribani jumla ya megawati 2115.
Akizungumza kwa niaba ya uongozi wa kituo, Kaimu Meneja Uendeshaji na Udhibiti wa Mifumo wa Kituo cha Kuzalisha Umeme cha Julius Nyerere, Mha. Elinainyi Kalalu, alisema ziara hiyo imekuwa na tija kwa kuwa imewapa fursa ya kujionea namna fedha za wananchi zinavyotumika na matokeo yake kurudi kwao kupitia huduma bora ya umeme.
“ Ziara hii imekuwa na tija kubwa , nipende kusisitiza kuwa, Kituo kitaendelea kuzalisha umeme kwa weledi na ufanisi ili kuhakikisha huduma ya uhakika kwa wananchi. Ni muhimu pia kwa TRA kuendelea kuhamasisha ulipaji wa kodi, kwani ndizo zinazoziwezesha Serikali kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo nchini ,” alisisitiza Mha. Kalalu.
Ziara hiyo imekuwa ya mafanikio kwani imeimarisha uelewa kuwa ulipaji wa kodi kwa hiari na kwa wakati ni msingi wa utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo, ikiwemo uwekezaji katika sekta muhimu ya nishati ya umeme, kwa ustawi wa Taifa.




