Kibaha, Pwani — Wizara ya Nishati imeanza kutoa mafunzo kwa Maafisa Dawati wa Nishati Safi ya Kupikia ngazi ya mikoa na halmashauri, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Mkakati wa Taifa wa Nishati Safi ya Kupikia.
Lengo la mafunzo hayo ni kuwajengea maafisa hao uelewa wa pamoja kuhusu utekelezaji wa mkakati huo, sambamba na kuwasaidia kutambua majukumu yao katika kusimamia ajenda ya nishati safi nchini.
Akifungua mafunzo hayo wilayani Kibaha mkoani Pwani, Mwakilishi wa Katibu Tawala wa Mkoa wa Pwani, Hadija Mruma, aliipongeza Wizara ya Nishati kwa jitihada zake za vitendo katika kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia nchini.
Amesema hatua ya kupeleka elimu na vifaa vya nishati safi hadi ngazi za mikoa, halmashauri na vijiji ni ushahidi wa dhamira ya Serikali kuhakikisha Watanzania wanatumia nishati salama na rafiki kwa mazingira.
“Mkoa wa Pwani umeendelea kuchukua hatua mbalimbali kuhakikisha wananchi wanatumia nishati safi ya kupikia katika taasisi na kaya.
Kwa sasa, takribani asilimia 76 ya taasisi zinazolisha watu zaidi ya 100 zimehamia kwenye matumizi ya nishati safi,” alisema Bi. Mruma.
Aidha, aliwapongeza Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kwa kushirikiana na Mkoa wa Pwani katika kuhamasisha matumizi ya nishati safi, ikiwemo utoaji wa mitungi ya gesi kwa bei ya ruzuku.

Mikoa Sita Ya Kwanza Yaanza Mafunzo
Kwa upande wake, Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Nishati Safi ya Kupikia kutoka Wizara ya Nishati, Ngereja Mgejwa, alisema mafunzo hayo yameanza kutolewa Kibaha, yakihusisha maafisa kutoka mikoa ya Pwani, Morogoro, Dar es Salaam, Mtwara, Lindi na Tanga.
Alibainisha kuwa mpango huo utahusisha pia mikoa mingine iliyosalia, kwani lengo la Serikali ni kuhakikisha elimu ya nishati safi ya kupikia inawafikia Maafisa Dawati wote katika mikoa 26 ya Tanzania Bara pamoja na halmashauri zake.
“Matumizi ya nishati safi ya kupikia ni kipaumbele cha nchi na dunia kwa ujumla, ili kupunguza athari za kiafya, kimazingira na kiuchumi zinazotokana na matumizi ya nishati hatarishi kama kuni na mkaa,” alisema Mgejwa.
Mawasiliano na Elimu kwa Umma
Naye, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano wa Wizara ya Nishati, Neema Mbuja, alisema mafunzo hayo yanahusisha pia elimu kuhusu Mkakati wa Taifa wa Mawasiliano wa Nishati Safi ya Kupikia.
Amesema mafunzo hayo yatasaidia maafisa dawati hao kujua mbinu bora za mawasiliano na namna ya kufikisha elimu kwa wananchi kuhusu faida za nishati safi.

“Ni muhimu maafisa dawati wakafahamu njia sahihi za mawasiliano na jumbe watakazotumia katika maeneo yao.
Mkakati wa Taifa wa Mawasiliano unatoa mwongozo wa ushirikiano kati ya wadau wote katika kutoa elimu na kuondoa dhana potofu kuhusu nishati safi,” alieleza Bi. Mbuja.
Aliongeza kuwa kupitia mkakati huo, Serikali na wadau wanatarajia kubadili mitazamo hasi ya wananchi kuhusu nishati safi na kuhimiza matumizi yake kama sehemu ya utekelezaji wa ajenda ya kitaifa ya kupikia kwa nishati safi.





