WMA yahimiza ushirikiano na sekta binafsi

OFISA Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Vipimo (WMA), Alban Kihulla, ametoa wito kwa taasisi, asasi na mashirika binafsi kuimarisha ushirikiano na wakala hiyo katika masuala yanayohusu vipimo kwa nyanja za biashara, afya, usalama na mazingira.

Kihulla alitoa wito huo juzi alipokuwa akizungumza na wahariri na waandishi wa vyombo mbalimbali vya habari katika mkutano ulioandaliwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina, jijini Dar es Salaam.

Akitoa taarifa ya utendaji kazi, majukumu na mafanikio ya WMA, alisema kuna maeneo 17 ambayo sekta binafsi inaweza kushirikiana na WMA ili kuongeza tija katika sekta ya vipimo.

Kihula akitaja baadhi ya maeneo hayo ya kivipimo kuwa ni ukaguzi na uhakiki wa mizani, uhakiki wa mitambo ya gesi, dira za maji zilizoko kwenye matumizi, mashine za michezo ya kubahatisha na lifti za majengo.

Kuhusu sheria inayoipa mamlaka WMA kutekeleza majukumu yake, Kihula alisema sheria hiyo ambayo msingi wake hasa ni vitabu vitakatifu vya dini, yaani  Quran na Biblia, ni ya Usimamizi wa Vipimo Sura Namba 245 na 340 ya Mwaka 2002 ambayo inawatambua maafisa vipimo kama wakaguzi wanapotekeleza majukumu ya ukaguzi na uhakiki wa vipimo.

Alibainisha kuwa jukumu kubwa la WMA ni kuilinda jamii ili kuepukana na madhara yatokanayo na matokeo ya upimaji usio sahihi katika biashara ambapo WMA inawajibika kukagua sehemu za biashara kama vile maduka ya kuuzia bidhaa mbalimbali, viwanda, maduka ya vifaa vya ujenzi, vituo vya kujazia mafuta na sehemu nyinginezo.

“Tunasisitiza kila mara kwa wananchi kuwa, ukihisi kwamba umepimiwa visivyo sahihi katika sehemu uliyoenda kupata huduma, ni jukumu lako kutoa taarifa ili wataalamu wetu wakafanye uchunguzi eneo hilo,” alisema. 

Mtendaji huyo mkuu aliongeza kuwa WMA inawajibika kuhakiki mzunguko mzima wa mafuta kuanzia yanapoingia nchini kupitia bandari, uhakiki wa matangi na maghala ya kuhifadhia mafuta na wakala hufanya shughuli hizo kupitia kitengo maalum cha bandari.

Sambvamba na hayo, Kihulla alibainisha kwamba WMA ina mpango wa kuingia kwenye maeneo mapya ya uhakiki wa vipimo kama vile uhakiki wa gharama za vifurushi vya muda wa maongezi na mashine za michezo ya kubashiri.

Mpango mwingine, alisema ni kutoa elimu kwa wananchi na wadau wa vipimo kuhusiana na matakwa ya sheria ya vipimo, kuendelea kuboresha mifumo ya utendaji kazi pamoja na kuwajengea uwezo zaidi wataalamu wake ikiwa ni kuwapa mafunzo zaidi na ununuzi wa vifaa vya kisasa.

Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile ameipongeza WMA kutokana na utendaji kazi wake na ameahidi ushirikiano wa vyombo vya habari na Wakala hiyo ili kuhakikisha elimu ya matumizi sahihi ya vipimo inawafikia wananchi kwa ukubwa wake.

“WMA mna nafasi ya kuufikia umma wa watanzania kwa kutumia vyombo vya habari kwenye kampeni hizi za kivipimo, elimu inahitajika sana, wananchi wanatakiwa kufahamu kwamba wanapaswa kuwa makini wanapokwenda kupata huduma mbalimbali, hii itachagiza maendeleo katika taifa letu” alisema.

WMA imeendelea kutoa elimu ya vipimo kwa wadau mbalimbali ambao ni pamoja na taasisi za umma na binafsi na pia kuwa mstari wa mbele katika kuchangia katika pato la taifa kupitia uwasilishaji wa gawio la serikali kwa Msajili wa Hazina.

Leave a Comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *