51,138 kufanya mtihani kumaliza elimu ya msingi Arusha 

Mtihani huo,utafanyika kwa siku mbili kuanzia Septemba 11 hadi 12 mwaka huu,kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na Baraza la Mitihani la Taifa.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Mkoa wa Arusha, Elinipa Lupembe,ilieleza kuwa kati ya watahiniwa 51,138 wavulana ni 24,937 na wasichana ni 26,201.

Kaimu Mkuu huyo wa Mawasilisho,alisema watahiniwa 9,095 kati ya watahiniwa wote, wanafanya mtihani kwa mfumo wa lugha ya kiingereza.

Aidha alisema katika shule hizo 801, shule za msingi 20 zitafanya mtihani huo kwa mara ya kwanza kukiwa na jumla ya wasimamizi wakuu 801 na wasimamizi wasaidizi wa mikondo 2320 na kila mkondo utakuwa na msimamizi mmoja.

Katika hatua nyingine, taarifa hiyo ilieleza serikali kupitia Baraza la Mitihani la Taifa limekamilisha taratibu zote za maandalizi kwa kuweka mazingira rafiki kwa kila mwanafunzi wakiwamo wenye mahitaji maalum kufanya mtihani huo.

Vilevile serikali imetoa rai kwa wazazi na walezi wenye watoto waliosajiliwa kufanya mtihani kuhakikisha kuwa watoto wote wanafika kwenye vituo vyao vya kufanyia mtihani kwa muda uliopangwa.

“Uongozi wa Mkoa wa Arusha,unawatakia kila kheri watahiniwa wa mtihani wa Darasa la Saba kwa mwaka 2024, na tunawakumbusha kuzingatia Sheria,kanuni na taratibu zote zilizowekwa na Baraza za Mitihani,”alisema.

Leave a Comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *