Spika wa Bunge la nchi ya Bhutan Sangay Dorji, ameipongeza Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kazi nzuri inayofanya ya uhifadhi wa maliasili na kutangaza utalii hatua inayoiwezesha Tanzania kuwa na vivutio vya asili hususani misitu.
Dorji ametoa pongezi hizo alipotembelea Banda la Wizara ya Maliasili na Utalii lililopo kwenye Mkutano wa 153 wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU, Jijini Arusha.
Akiwa ameambatana na maafisa mbalimbali wa Bunge hilo, Dorji alipata nafasi ya kupata maelezo mbalimbali kutoka kwa maafisa wa Wizara ya Maliasili na Utalii pamoja na wadau wa Sekta za Utalii na Uhifadhi nchini kuhusu maendeleo ya sekta hizo muhimu katika ukuzaji wa uchumi.
Aidha ameahidi kuwa balozi wa kuelezea uzuri wa Tanzania nchini Bhutan ili wananchi wa nchi hiyo wafanye safari kuja Tanzania kushuhudia utajiri wa urithi wa vivutio vilivyopo.
Pamoja na kiongozi huyo, Banda hilo linaloratibiwa na Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) limeendelea kutembelewa na wageni mbalimbali wa mkutano huo ili kujipatia huduma za Uhifadhi na Utalii.




