Timu za Mwitikio wa Haraka (RRTs) mkoani Iringa zimeimarisha uwezo wa kukabiliana na dharura za afya, ikiwamo milipuko ya magonjwa ya kuambukiza, kupitia zoezi la majaribio la kukabiliana na Ebola.
Zoezi hilo limefanyika jana, Oktoba 6, 2026, kwa ushirikiano wa Wizara ya Afya na Shirika la Afya Duniani (WHO), likilenga kupima uwezo wa timu hizo katika kutambua, kuchunguza, kuripoti na kutoa mwitikio kwa wakati pale linapotokea tukio linalohisiwa kuwa la Ebola.
Aidha, zoezi hilo limehusisha wataalamu kutoka sekta na ngazi mbalimbali kwa lengo la kuimarisha uratibu na ushirikiano wakati wa kukabiliana na dharura za afya.
Kupitia zoezi hilo, wataalamu wamejengewa uwezo katika ufuatiliaji wa magonjwa, epidemiolojia, huduma za maabara, kinga na udhibiti wa maambukizi, afya ya mazingira pamoja na matumizi sahihi ya vifaa kinga binafsi (PPE).
Wizara ya Afya imesema hatua hiyo ni sehemu ya juhudi za kuimarisha mifumo ya ufuatiliaji na mwitikio wa dharura za afya, ili kuwezesha milipuko ya magonjwa kutambuliwa mapema na hatua stahiki kuchukuliwa kwa wakati.




