Sunday, December 7, 2025
spot_img
HomeHabariDk. Nchimbi amshukuru Dk. Mpango kwa mchango wake

Dk. Nchimbi amshukuru Dk. Mpango kwa mchango wake

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi, amempongeza na kumshukuru Makamu wa Rais Mstaafu, Mhe. Dkt. Philip Mpango, kwa mchango mkubwa alioutoa katika kumsaidia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika kipindi cha kwanza cha Serikali ya Awamu ya Sita.

Dkt. Nchimbi alitoa pongezi hizo wakati wa hafla ya makabidhiano ya Ofisi ya Makamu wa Rais iliyofanyika katika Ikulu ya Chamwino, mkoani Dodoma, ambapo alitambua juhudi na uadilifu uliomsaidia Rais kufanikisha utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo nchini.

Amesema kazi kubwa iliyotekelezwa katika kipindi cha kwanza cha Awamu ya Sita imechangia kwa kiasi kikubwa kurahisisha kampeni za Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, kutokana na mafanikio yaliyopatikana chini ya uongozi wa Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Ninathamini kwa dhati mchango mkubwa wa Dkt. Mpango katika kuimarisha Ofisi ya Makamu wa Rais na kusaidia utekelezaji wa sera mbalimbali za serikali. Mimi nitaendeleza juhudi hizo kwa uwezo wangu wote kumsaidia Mhe. Rais katika kuwaletea Watanzania maendeleo,” alisema Dkt. Nchimbi.

Aidha, amemuomba Dkt. Mpango kuendelea kutoa ushauri na mchango wake pale utakapohitajika, hususan katika utekelezaji wa sera za maendeleo ikiwemo masuala ya uchumi wa buluu.

Kwa upande wake, Makamu wa Rais Mstaafu Dkt. Philip Mpango alimpongeza Dkt. Nchimbi kwa kuteuliwa kushika nafasi hiyo muhimu na kumtaka atekeleze majukumu yake kwa hekima, unyenyekevu na uadilifu, akisisitiza kuwa nafasi hiyo ni ya kuhudumia wananchi kwa moyo wa uzalendo na uwajibikaji.

Dkt. Mpango pia aliahidi kuendelea kushirikiana na serikali pale atakapohitajika, ili kuhakikisha maendeleo na ustawi wa Taifa vinaendelea kuimarika.

RELATED ARTICLES

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisment -
NMB Tanzania

Most Popular

Recent Comments