
Waziri wa Maji Jumaa Aweso ameweka jiwe la msingi katika mradi wa maji wa Bwanga uliopo wilayani Chato mkoani Geita baada ya kuridhishwa na utekelezaji wa kazi nzuri iliofanyika na kuipongeza RUWASA Geita inayoongozwa na mhandisi Jabiri Kayilla kwa kazi nzuri na kubwa waliofanya katiks mradi huu na miradi mingine ya Maji.
Waziri Aweso ametumia nafasi hiyo kumuagiza Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji Mhandisi Mwajuma Waziri kuhakikisha anawapa Shilingi milioni 10 RUWASA Mkoa wa Geita ambayo itagawiwa kwa watumishi wote kama motisha ili kuongeza morali ya kazi huku akiwataka watumishi wengine wa mamlaka za maji nchini kuiga mfano mzuri unaofanywa na RUWASA Mkoa wa Geita.
Aidha Waziri Aweso ametoa pongezi kuhusiana na Vyombo vya Watumiaji Maji (CBWSOs) kujiunga na mfumo wa makusanyo wa GePG lakini akaelekeza kuwa mfumo huo usiwe kikwazo katika kutoa huduma ya maji yenye tija kwa wananchi kwa wakati kwani hilo ndio lengo la msingi la Wizara ya Maji.


Awali akimkaribisha Waziri wa Maji Aweso katika Mradi huo Meneja wa RUWASA Mkoa wa Geita Mhandisi Jabiri Kayilla amesema mradi huo umetekelezwa na mkandarasi Otonde Constraction Company Ltd kwa thamani ya shilingi Bilioni 1.6 na utanufaisha zaidi ya elfu 27 ambapo ujenzi umefikia asilimia 99 na wananchi wameshaanza kupata huduma ya maji safi na salama.
Akizungumza kwa niaba ya wananchi wa Chato Mbunge wa Jimbo la Chato Dkt. Medard Kalemani ameipongeza serikali kwa kutekeleza mradi huo kwani kabla ya ujenzi wa mradi huo wananchi walikuwa wanahangaika kufuata maji umbali mrefu.


