Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge amesema eneo la Kongani Viwanda la Misugusugu, Manispaa ya Kibaha ni mradi muhimu katika kuimarisha uchumi wa Mkoa wa Pwani na kuongeza fursa za ajira kwa wananchi.
Kunenge amesema kitendo cha Manispaa ya Kibaha kutenga eneo lenye ukubwa wa hekta 350 kwa ajili ya kuanzisha Kongani Mpya ya Viwanda ni chakupongezwa hatua ambayo itasaidia kuzalisha ajira.
Pia amesema kuanzishwa kongani hiyo Manispaa imetekeleza maagizo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo aliyaagiza.
“Na hili la mradi wa eneo la maegesho ya magari makubwa ya mizigo katika eneo la Misugusugu, ni mradi wa kimkakati utakaosaidia kuondoa changamoto ya magari makubwa kuegeshwa kando ya barabara”,amesrma Kunenge.

Amesema mradi huo wa kimkakati wa eneo la maegesho ya magari utasaidia kuongeza usalama barabarani na kutoa huduma muhimu kwa viwanda vitakavyoanzishwa ndani ya kongani hiyo.
Mkuu huyo wa mkoa amezielekeza taasisi wezeshi ikiwemo TANROADS,TARURA, TANESCO, DAWASA na TTCL, kuhakikisha zinaimarisha na kukamilisha miundombinu muhimu katika eneo hilo la kongani ya viwanda ili kuvutia wawekezaji na kuwezesha shughuli za uzalishaji kuanza mapema.
Amesema ushirikiano wa karibu kati ya Serikali, halmashauri na taasisi mbalimbali ni msingi wa kufanikisha utekelezaji wa mradi huo, ambao unatarajiwa kuwa kichocheo kikubwa cha maendeleo ya viwanda na uchumi wa Mkoa wa Pwani pamoja na Taifa kwa ujumla.
Awali, akitoa taarifa ya mradi Mkurugenzi wa Manispaa ya Kibaha, Dk. Rogers Shemwelekwa, amesema eneo hilo tayari lina huduma muhimu za maji na umeme, jambo linalolifanya kuwa kivutio kwa wawekezaji wa viwanda mbalimbali ikiwemo vya kutengeneza viatu na nguo.
Dk. Shemwelekwa amesema kupitia kongani hiyo, Manispaa inatarajia kuzalisha zaidi ya ajira 1,000, kuongeza mapato ya Serikali na Halmashauri pamoja na kuimarisha shughuli za uzalishaji na biashara katika Manispaa ya Kibaha.
Kwa upande wa mradi wa maegesho ya magari makubwa, Mkurugenzi huyo amesema huduma imeanza kutolewa Julai mosi mwaka huu na hadi sasa magari 90 huingia na kuegeshwa kila siku katika eneo hilo.





