HomeAfyaJukwaa la Win & Learn Academic latimiza miaka 20, tafiti za Afya zang'ara MUHAS

Jukwaa la Win & Learn Academic latimiza miaka 20, tafiti za Afya zang’ara MUHAS

KWA zaidi ya miongo miwili, jukwaa la Win & Learn Academic Event limekuwa zaidi ya mashindano ya wanafunzi. Limekuwa kiwanda cha kuzalisha watafiti, wabunifu na viongozi wa sekta ya afya ambao leo wanachangia kutatua changamoto za afya nchini na nje ya mipaka ya Tanzania.

Lilianzishwa mwaka 2006 na wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS), Win & Learn Academic Event leo limeadhimisha miaka 20 ya mafanikio, likiwa limepanua wigo wake na kushirikisha wanafunzi kutoka vyuo mbalimbali vya afya nchini.

Katika maadhimisho hayo, viongozi wa chuo, wahitimu na wanafunzi walitumia jukwaa hilo kutafakari mchango wake katika kukuza utafiti, ubunifu na kuandaa kizazi kipya cha wataalamu wa afya wanaoweza kutoa suluhisho kwa changamoto zinazoikabili Tanzania na dunia.

Prof. Sunguya: Tumewalea watafiti wengi kupitia Winning Line

Naibu Makamu Mkuu wa MUHAS anayeshughulikia Utafiti na Ushauri wa Kitaalamu (DVC-RC), Prof. Bruno Sunguya, amesema jukwaa hilo limekuwa sehemu muhimu ya kuwajenga wanafunzi kuwa watafiti mahiri tangu wakiwa chuoni.

Amesema viongozi wengi wa tafiti na wataalamu wa afya wanaotambulika leo waliwahi kusimama katika jukwaa hilo wakitambulisha tafiti zao kwa mara ya kwanza.

Prof. Sunguya amesema hata yeye binafsi alishiriki katika toleo la kwanza mwaka 2006 akiwa mwanafunzi, jambo lililomjengea kujiamini, uwezo wa kushindana kitaaluma na msingi wa taaluma yake ya utafiti.

“Winning Line si mashindano ya kawaida. Hapa wanafunzi wanajifunza kufikiri kisayansi, kujenga hoja kwa ushahidi, kuwasilisha tafiti zao mbele ya majaji na kujifunza kutoka kwa wenzao. Hapo ndipo viongozi wa kesho wa tafiti wanapozaliwa,” amesema.

Ameeleza kuwa kupitia jukwaa hilo wanafunzi pia hujifunza uongozi, uandishi wa mapendekezo ya miradi ya utafiti, kutafuta fedha za tafiti na kujenga ushirikiano na wataalamu kutoka taaluma mbalimbali.

Kwa mujibu wake, uwezo huo ndio unaowafanya wahitimu wengi wa MUHAS kuendelea kufanya tafiti zenye athari chanya katika sekta ya afya.

Prof. Sunguya amewataka wanafunzi kuelekeza nguvu zaidi kwenye tafiti zinazohusu teknolojia mpya, matumizi ya akili bandia (AI), afya ya kidijitali pamoja na magonjwa yasiyoambukiza kama saratani, kisukari, shinikizo la damu, magonjwa ya moyo na afya ya akili.

“Changamoto za afya zimebadilika. Leo tunahitaji tafiti zinazotoa majibu ya kesho, si yale ya jana pekee,” amesema.

Marsha Macatta: Mawazo ya wanafunzi yasibaki maktabani

Mgeni rasmi wa maadhimisho hayo, Marsha Macatta Yambi, ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa Baraza la MUHAS na Rais wa Jumuiya ya Wahitimu wa MUHAS (MUHAS Convocation), amesema Win & Learn Academic Event limekuwa jukwaa la kugeuza mawazo ya wanafunzi kuwa suluhisho halisi kwa jamii.

Amesema lengo la jukwaa hilo si kuwafanya wanafunzi wasubiri kuhitimu ndipo waanze kutatua matatizo ya jamii, bali kuwajengea uwezo wa kubuni suluhisho wakiwa bado chuoni.

Kwa mujibu wake, mafanikio ya bunifu mbalimbali zilizotoka kwenye jukwaa hilo ni uthibitisho kuwa wanafunzi wana uwezo wa kuleta mageuzi makubwa katika sekta ya afya endapo watapata mazingira na ushirikiano unaofaa.

Ametaja mifumo ya Saratani AI na Dawa Mkononi kuwa miongoni mwa bunifu zilizoanzia katika Winning Line kabla ya kukua na kupata kutambulika ndani na nje ya Tanzania.

“Mawazo ya wanafunzi yasibaki kwenye makabrasha ya maktaba. Tunataka yawe bidhaa, yawe huduma na yawe suluhisho la changamoto za wananchi,” amesema.

Macatta alisema dunia ya sasa inahitaji ubunifu unaochanganya afya, teknolojia, mabadiliko ya tabianchi na maendeleo ya kijamii, akisisitiza kuwa wataalamu wa afya wa kizazi kipya wanapaswa kufikiri nje ya mifumo ya kawaida.

Aidha, amewataka wadau wa maendeleo, sekta binafsi na taasisi mbalimbali kuwekeza zaidi katika bunifu za wanafunzi ili kuzisaidia kufikia hatua ya kutumika kwa jamii.

Amesema mwaka huu jukwaa limepokea bunifu zaidi ya 100 zenye thamani ya takribani Sh milioni 27, jambo linaloonyesha uwezo mkubwa uliopo miongoni mwa vijana.

Mwanafunzi: Tafiti zetu zinaweza kubadili sera

Kwa upande wake, mwanafunzi wa mwaka wa tano wa udaktari MUHAS, Emmanuela Samwel Maira, amesema jukwaa hilo limewapa wanafunzi ujasiri wa kuamini kuwa tafiti wanazofanya zinaweza kuleta mabadiliko katika sekta ya afya.

Maira amewasilisha utafiti unaochunguza namna dalili zinazowapata wanawake kabla ya hedhi zinavyoathiri uwezo wao wa kujifunza, kufanya kazi na kutekeleza majukumu ya kila siku.

Amesema licha ya tatizo hilo kuwaathiri wanawake wengi, bado halijapewa uzito unaostahili katika mijadala ya afya na elimu.

“Kupitia Winning Line tunapata nafasi ya kukutana na wataalamu, kupokea ushauri na kuona namna tafiti zetu zinavyoweza kutumika kuboresha sera na huduma za afya,” amesema.

Ametaja changamoto kubwa inayowakabili wanafunzi kuwa ni kukosa kujiamini na kuhisi tafiti zao hazina mchango mkubwa kwa jamii.

Hata hivyo, amesema jukwaa hilo limewafanya waamini kuwa mawazo yao yana thamani na yanaweza kuendelezwa hadi kufikia hatua ya kutatua changamoto za wananchi.

Erick Mahatara: Ushirikiano ndio msingi wa tafiti

Naye Rais wa Serikali ya Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Afya KCMC, Erick Mahatara, amesema Winning Line limekuwa daraja la kuunganisha wanafunzi kutoka vyuo mbalimbali vya afya nchini.

Amesema kupitia jukwaa hilo wanafunzi kutoka MUHAS, KCMC, St. Francis, Hubert Kairuki, St. Joseph na taasisi nyingine hukutana, huwasilisha tafiti zao na kujifunza kutoka kwa wenzao.

Kwa mujibu wake, mazingira hayo yanawajengea uzoefu, mtandao wa kitaaluma na ushirikiano ambao utakuwa msingi wa tafiti kubwa wanazotarajia kufanya baada ya kuhitimu.

“Hakuna mtafiti anayefanikiwa peke yake. Tafiti za kisasa zinahitaji ushirikiano wa taaluma mbalimbali. Winning Line ndiyo sehemu ambayo ushirikiano huo unaanza kujengwa,” alisema.

Amesema mitandao inayoundwa kupitia jukwaa hilo ndiyo itakayowezesha kizazi cha sasa cha wanafunzi kuwa watafiti wakubwa na viongozi wa kesho katika sekta ya afya.

Jukwaa lililovuka mipaka ya MUHAS

Tofauti na lilivyoanza mwaka 2006 likiwashirikisha wanafunzi wa MUHAS pekee, Win & Learn Academic Event sasa limekuwa jukwaa la kitaifa linalowakutanisha wanafunzi kutoka vyuo mbalimbali vya afya nchini.

Kwa miaka 20, limeendelea kuwa sehemu ya kuibua tafiti, ubunifu na suluhisho zinazolenga kuboresha afya za Watanzania, huku viongozi wa MUHAS wakisisitiza kuwa hatua inayofuata ni kuongeza ushirikiano na sekta binafsi, taasisi za maendeleo na wadau wa kimataifa ili mawazo ya wanafunzi yaweze kuendelezwa kutoka ngazi ya darasani hadi kuwa teknolojia, sera na huduma zinazobadili maisha ya wananchi.

Kwa washiriki wa maadhimisho hayo, Win & Learn Academic Event si tu historia ya miaka 20 ya mashindano ya kitaaluma, bali ni historia ya kuzaliwa kwa kizazi kipya cha watafiti na wabunifu wanaotarajiwa kuiongoza Tanzania katika kutafuta suluhisho la changamoto za afya za sasa na zijazo.

RELATED ARTICLES

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisment -
NMB Tanzania

Most Popular

Recent Comments