HomeAfyaTanzania yaibuka kitovu kipya cha afya Afrika Mashariki

Tanzania yaibuka kitovu kipya cha afya Afrika Mashariki

DAR ES SALAAM: Tanzania inaendelea kuimarisha nafasi yake kama kitovu kinachochipukia cha uzalishaji wa bidhaa za afya katika Afrika Mashariki, huku juhudi za Serikali kuongeza uzalishaji wa ndani wa dawa, vifaa tiba na bidhaa nyingine muhimu za afya zikishika kasi.

Hatua hiyo inaenda sambamba na mikakati ya kuvutia uwekezaji zaidi katika sekta ya afya na kupunguza utegemezi wa bidhaa zinazoagizwa kutoka nje ya nchi, hali inayotarajiwa kuchochea biashara ya bidhaa za afya ndani ya ukanda wa Afrika Mashariki.

Mwelekeo huo unaakisi jitihada zinazofanywa na nchi mbalimbali za Afrika Mashariki kuimarisha mifumo ya afya, kuongeza uwezo wa uzalishaji wa ndani na kujenga minyororo imara ya usambazaji wa bidhaa za afya.

Katika mpangilio huo, Tanzania inazidi kujenga uwezo katika uzalishaji wa bidhaa za afya, huku Kenya ikiendelea kuwa kitovu muhimu cha usafirishaji na usambazaji wa bidhaa katika ukanda huo. Ushirikiano huo unarahisisha biashara ya kuvuka mipaka na kuwapa wazalishaji, wasambazaji, hospitali na wawekezaji fursa ya kuhudumia masoko mapana zaidi.

Takwimu zinaonyesha kuwa soko la afya na ustawi Afrika Mashariki linakadiriwa kufikia thamani ya dola za Marekani bilioni 16.8 mwaka 2025 na linatarajiwa kukua hadi dola bilioni 23.6 ifikapo mwaka 2034. Aidha, soko la hospitali linakadiriwa kuwa na thamani ya dola bilioni 9.25, huku soko la dawa likifikia dola bilioni 2.39 mwaka 2025.

Ukuaji huo unaashiria kuongezeka kwa mahitaji ya huduma za afya, vifaa tiba, teknolojia za kisasa na mifumo bora ya usambazaji katika ukanda huo.

Katika hatua nyingine, viongozi na wadau wa sekta ya afya kutoka Afrika Mashariki na maeneo mbalimbali duniani wanatarajiwa kukutana katika maonesho ya WHX Nairobi, yatakayofanyika Septemba 16 hadi 18, 2026, katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Kenyatta (KICC), Nairobi.

Maonesho hayo, ambayo yanafanyika kwa mara ya 10 mwaka huu, yatawakutanisha wazalishaji, wasambazaji, viongozi wa hospitali, wataalamu wa ununuzi, kampuni za usafirishaji na watunga sera kwa ajili ya kujadili fursa za biashara, uwekezaji na ushirikiano katika sekta ya afya barani Afrika.

WHX Nairobi, ambayo awali ilijulikana kama Medic East Africa, inafanyika chini ya udhamini wa Wizara ya Afya ya Kenya. Toleo la mwaka huu linatarajiwa kuvutia zaidi ya washiriki 5,500, huku takribani asilimia 40 wakitarajiwa kutoka nje ya Kenya.

Aidha, zaidi ya waoneshaji 200 kutoka zaidi ya nchi 30 wanatarajiwa kushiriki, huku eneo la maonesho likipanuliwa hadi kufikia mita za mraba 4,500, sawa na ongezeko la asilimia 81 ikilinganishwa na mwaka uliopita. Maonesho ya mwaka 2025 yalizalisha biashara yenye thamani inayokadiriwa kufikia dola za Marekani milioni 84.1.

Akizungumzia mwenendo huo, Tom Coleman, Mkurugenzi wa Kanda wa Sekta ya Afya wa inD, amesema sekta ya afya Afrika Mashariki inaendelea kuwa ya kikanda zaidi kadri nchi zinavyoongeza uwekezaji katika uzalishaji wa ndani na kuimarisha biashara pamoja na mifumo ya usambazaji.

Amesema juhudi za Tanzania kupanua uzalishaji wa dawa na vifaa tiba, zikisaidiwa na uwezo wa Kenya katika usafirishaji na usambazaji, zinajenga soko lililounganishwa zaidi katika Afrika Mashariki.

“Ushirikiano wa kikanda utakuwa muhimu katika kuongeza upatikanaji wa dawa, teknolojia za afya na huduma bora kwa mamilioni ya wananchi katika ukanda huu,” amesema.

Toleo la mwaka 2026 la WHX Nairobi litaangazia ubunifu katika maeneo mbalimbali ya sekta ya afya, ikiwemo vifaa tiba, teknolojia za uchunguzi na maabara, mifumo ya afya ya kidijitali, miundombinu ya afya, huduma za afya na bidhaa zinazotumika hospitalini.

Kadri sekta ya afya Afrika Mashariki inavyoendelea kukua, maonesho hayo yanatarajiwa kuwa jukwaa muhimu la kuimarisha ushirikiano wa kibiashara, uwekezaji na ubadilishanaji wa teknolojia, huku Tanzania ikitumia nafasi yake inayokua katika uzalishaji wa bidhaa za afya kuongeza ushiriki wake katika soko la kikanda.

RELATED ARTICLES

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisment -
NMB Tanzania

Most Popular

Recent Comments