
Waziri wa Madini, Anthony Mavunde ametangaza kukamatwa kwa madini ya dhahabu kilo 15.78 bandarini yalipokuwa yakitoroshwa.
Ameyasema hayo leo Septemba,11, 2024 Jijini Dar es Salaam alipokutana na alipozungumza na vyombo vya habari kuuhabarisha umma wa Watanzania juu ya tukio hilo.
“Nchi yetu inazo sekta kadhaa za uzalishaji ambazo mapato yake ndiyo msingi wa maendeleo ya uchumi wetu ikiwemo sekta ya madini. Sasa basi, tunapokuwa na watu wachache ambao wanajihusisha na shughuli hizi za utoroshaji wa madini na hivyo kuikosesha Serikali mapato hatuwezi kuwavumilia.”


“Kilo hizo 15.78 kwa bei ya leo zina thamani ya takribani bilioni 3.4, fedha ambazo kwa sasa zote watoroshaji hawa wanakwenda kuzipoteza. Serikali tunakwenda kufuta leseni zao wakitiwa hatiani na mahakama na kuwaweka kwenye orodha ambayo hawataruhusiwa kumiliki Leseni ya kufanya biashara yeyote katika mnyororo wa thamani wa madini nchini Tanzania,” amebainisha Mavunde.

Kwa mujibu wa mahojiano ya awali wakati uchunguzi unaendelea, watuhumiwa wamesema madini hayo ya dhahabu walikuwa wanasafirisha kutoka bandari ya Dar es Salaam kuelekea Visiwani Zanzibar.
