Mtibwa Sugar kuanza Ligi Kuu Sept. 20

TIMU ya Mtibwa Sugar iliyoshuka daraja msimu uliopita, itaanza kampeni yake ya kutaka kurejea Ligi Kuu Tanzania Bara nyumbani, Septemba 20, mwaka huu, katika Uwanja wa Manungu uliopo Turiani, Morogoro, itakapowavaa Maafande wa Green Warriors katika mchezo huo wa ufunguzi wa Ligi ya Championship.

Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa jana na Shirikisho la Mpira wa Miguu (TFF), inayoonesha kuanza kwa ligi hiyo, Septemba 20, timu nyingine iliyoteremka daraja msimu huu, Geita Gold nayo itakuwa nyumbani Septemba 21 katika Uwanja wa Nyankumbu, Geita kukipiga na TMA.

Katika ratiba hiyo inaonesha kuwa kutakuwa na mechi mbili za ufunguzi, ambapo mbali na Mtibwa dhidi ya Green Warriors, mechi nyingine siku hiyo itakuwa ni kati ya Mbeya City itakayocheza uwanja wake wa nyumbani, Sokoine Mbeya, dhidi ya Bigman FC, ambayo zamani ilijulikana kwa jina la Mwadui FC.

Septemba 21 pia kutakuwa na michezo mitatu, ambapo mbali na Geita Gold dhidi ya TMA, pia kwenye Uwanja wa Mabatini, Mlandizi mkoani Pwani, Cosmopolitan itaialika African Sports, ambapo Songea United itakuwa nyumbani, Uwanja wa Majimaji kuvaana na Mbeya Kwanza.

Mechi zingine tatu za kumalizia raundi ya kwanza zinatarajiwa kupigwa Septemba 22, pale Polisi Tanzania itakapocheza dhidi ya Mbuni kwenye Uwanja wa Ushirika, Moshi, huku Biashara United ikiwa Uwanja wa Karume, Musoma, Mara dhidi ya Transit Camp, wakati Kiluvya FC yenyewe itashuka Dimba la Mabatini, Mlandizi kupepetana na Stand United.

Ratiba inaonesha kuwa raundi ya pili itapigwa Septemba 27, wakati Stand United itakapoikaribisha Transit Camp, Uwanja wa Kambarage, Shinyanga, Cosmopolitan dhidi ya Mtibwa Sugar Uwanja wa Mabatini, Mbeya City dhidi ya Mbeya Kwanza katika dimba la Sokoine.

Septemba 28, mwaka huu, Green Warriors itakipiga dhidi ya African Sports, Mabatini, Polisi Tanzania dhidi ya TMA Uwanja wa Ushirika,  Biashara United dhidi ya Kiluvya, Karume, na Septemba 29, raundi itahitimishwa kwa mchezo kati ya Songea United dhidi ya Bigman FC.

Chanzo: Nipashe

Leave a Comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *