
NYOTA wa Real Madrid, Rodrygo amesema Brazil inamhitaji Neymar ikiwa wanataka kufukuzia rekodi ya kutwaa Kombe la Dunia kwa mara ya sita mwaka 2026.
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 23, ambaye alifunga bao la kipindi cha kwanza na kusaidia Brazil kuishinda Ecuador 1-0 Ijumaa na kusimamisha msururu wao wa kupoteza mechi tatu mfululizo katika CONMEBOL za kufuzu Kombe la Dunia la 2026, alisema Neymar ni muhimu kwa mafanikio ya Brazil.
“Yeye ni nyota wetu, mchezaji wetu bora,” alisema Rodrygo katika mahojiano na ESPN Brasil.
“Mtu yeyote anaweza kuiona, ni kiasi gani amekosa. Kuwa na Neymar mwenye afya, jambo ambalo sote tunataka, na yuko katika hatua za mwisho za kupona kwake. Tunataka arejeshwe haraka iwezekanavyo.”
Mabingwa mara tano wa dunia, Brazil walipoteza mechi mfululizo dhidi ya Uruguay, Colombia na Argentina mwishoni mwa mwaka jana na walikuwa katika nafasi ya sita kwenye msimamo baada ya raundi sita.
Kwa ushindi huo wa Ijumaa, Brazil sasa wana pointi 10 na wako katika nafasi ya nne na jana Jumanne walitarajiwa kucheza na Paraguay mjini Asuncion.
Mfungaji bora wa muda wote wa Brazil kwa upande wa wanaume, Neymar alifanyiwa upasuaji wa kurekebisha kano za mbele katika goti lake la kushoto Novemba 2, 2023 nchini Brazil.
Amekuwa majeruhi kwa muda mrefu, ikiwa ni pamoja na majeraha kadhaa ya kifundo cha mguu wa kulia, ambayo yalimlazimu kukosa kucheza kwa wiki sita mnamo 2021 na kampeni ya ushindi ya Brazil ya Copa America 2019.
Rodrygo alisema kuwa anaendelea kuwasiliana na Neymar na kwamba anamchukulia kama mtu muhimu zaidi.
“Kila mara tunatuma ujumbe kila mmoja. Sasa anarejea kwenye mazoezi na kundi,” alisema Rodrygo.
“Ni mchezaji mwenzangu, inanisikitisha sana ninapoona mtu anamsema vibaya kwa sababu ya jinsi alivyo, huwa ananitumia ujumbe, ananisaidia, nampenda.”
Rodrygo alifunga mabao 10 katika mechi 34 za LaLiga msimu uliopita, na pia kuzifumania nyavu mara tano kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Nafasi yake katika timu ya Real Madrid imekuwa chini ya shinikizo baada ya kuwasili kwa Kylian Mbappe, ingawa kocha Carlo Ancelotti ameendelea kumchagua kama sehemu ya safu ya ushambuliaji ya wachezaji watatu hadi sasa katika kampeni hii.