
Bunge limeipongeza serikali kwa kujenga ofisi na maabara ya Tume ya Nguvu za Atomu Tanzania (TAEC), mionzi visiwani Zanzibarjambo litakalosaidia upimaji wa sampuli na kusaidia watafiti kuitumia maabara hiyo.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo, Husna Sekiboko, ametoa pongezi hizo leo wakati wa ziara ya kamati yake ilipotembelea ofisi na maabara za TAEC, zilizojengwa eneo la Dunga Zuze, Zanzibar.
Ujenzi wa maabara hiyo na ofisi umekamilika na kinachoendelea ni ununuzi wa vifaa vya maabara
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia, Omary Kipanga, amesema katika mchakato wa uzalishaji bidhaa pamoja na chakula, suala la mionzi haliwezi kuepukika kwa kuwa vyakula vinavyozalishwa nchini na vinavyotoka nje ya nchi, ni lazima viratibiwe vizuri ili visiwe na athari za mionzi.
Amesema ujenzi wa maabara ya upimaji wa mionzi Zanzibar kunaimarisha usalama wa wananchi pamoja na mazingira.

Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Nguvu za Atomu Tanzania (TAEC) Prof. Najat Kassim Mohammed, amesema ofisi na maabara zimejengwa eneo la kimkakati la viwanda hivyo bidhaa zinazohitaji kupimwa mionzi zitapimwa katika maabara hiyo jambo litakalorahisisha utendaji.
Kamati ya kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo, inetembelea miradi mbalimbali ya kimkakati nchini kwa lengo la kuona matumizi ya fedha zinazotolewa na serikali baada ya kupitishwa na bunge.