HomeHabariTANESCO yatwaa tuzo nne za mawasiliano

TANESCO yatwaa tuzo nne za mawasiliano

Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) limefanikiwa kutwaa tuzo nne za umahiri katika mawasiliano kwa umma, ikiwa ni kutambua mchango wake katika kuboresha eneo la utoaji wa taarifa, kuimarisha mawasiliano ya kimkakati na kutumia ubunifu katika kuwafikishia wananchi taarifa kwa ufanisi.

Akizungumza Kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO Bw Lazaro Twange mara baada ya kupokea tuzo hizo Oktoba 8, 2026, katika Mkutano wa Mwaka wa Chama cha Maafisa Uhusiano na Mawasiliano Tanzania (PRST), Mkurugenzi wa Mawasiliano na Huduma kwa Wateja wa TANESCO, Bi. Irene Gowelle, amesema mafanikio hayo ni heshima kubwa kwa Shirika na chachu ya kuendelea kubuni njia bora za mawasiliano pamoja na kuimarisha matumizi ya mifumo ya kidijitali katika utoaji wa huduma kwa wananchi.

Amesema TANESCO itaendelea kutumia teknolojia na majukwaa ya kidijitali kuhakikisha wananchi wanapata taarifa sahihi, kwa wakati na kwa njia rahisi, za kisasa na zenye ufanisi.

“Kwanza naishukuru sana PRST kwa kutambua mchango wa TANESCO katika mawasiliano kwa umma. Mafanikio haya yametokana na ushirikiano mkubwa tunaoupata kutoka Wizara ya Nishati, Bodi ya Wakurugenzi na Menejimenti ya TANESCO. Tunamshukuru pia Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuwekeza katika sekta ya umeme kwa kuimarisha miundombinu ya upatikanaji wa umeme na matumizi ya teknolojia zinazotusogeza karibu zaidi kwenye kuwahudumia wananchi,” amesema Bi. Gowelle.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Utawala na Usimamizi wa Rasilimali Watu kutoka Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Bi. Savera Kazaura, aliyemwakilisha Waziri wa Wizara hiyo, ameipongeza TANESCO kwa mafanikio hayo na kwa hatua kubwa iliyopiga katika kuboresha utoaji wa taarifa kwa wananchi, hususan wakati wa changamoto za huduma ya umeme.

Amesema taasisi za umma zinapaswa kuendelea kuwekeza katika mawasiliano ili kuongeza uelewa kwa wananchi na kuimarisha uhusiano kati ya serikali na jamii.

“Nawapongeza sana TANESCO kwa mafanikio haya. Shirika limeonyesha mabadiliko makubwa katika utoaji wa taarifa kwa wananchi kuhusu changamoto za umeme zinapojitokeza. Jitihada hizi zinapaswa kuendelezwa ili kuongeza imani ya wananchi na kuboresha zaidi utoaji wa huduma,” amesema Bi. Kazaura.

Katika tuzo hizo zilizoandaliwa na PRST, TANESCO ilitunukiwa Tuzo ya Ubora katika Usimamizi wa Mawasiliano wakati wa Migogoro (Crisis Communication Management), Tuzo ya Ubora katika Kampeni ya Elimu kwa Umma (Public Awareness Campaign) kupitia kampeni ya Nishati Safi ya pika kwa Umeme, pamoja na Tuzo ya Idara Bora ya Uhusiano na Mawasiliano kwa Umma (Best Public Relations Department).

Aidha, Bi. Irene Gowelle alitangazwa mshindi wa Tuzo ya Mtaalamu Bora wa Uhusiano na Mawasiliano kwa Umma Tanzania kwa mwaka 2026 (Best PR Practitioner 2026).

Tuzo hizo hufanyika kila mwaka zikilenga kuonesha mchango wa mawasiliano kwenye kuimarisha sekta mbalimbali na namna zinaongeza tija kwa wataalamu wa mawasiliano nchini.

RELATED ARTICLES

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisment -
NMB Tanzania

Most Popular

Recent Comments