Ufanisi TPA wazidi kuiweka pazuri ikipokea tuzo kwa Rais

MAMLAKA ya Bandari Tanzania (TPA), imepewa tuzo ya mshindi wa tatu kati ya Mashirika ya Umma yanayojiendesha kibiashara kwa ufanisi wa huduma na ukusanyaji wa mapato.

Rais Samia Suluhu Hassan ndiye aliyekabidhi tuzo hiyo leo jijini Arusha katika kikao Kazi cha Wenyeviti wa Bodi pamoja na Wakuu wa Taasisi wa Mashirika ya Umma na Wakala wa Serikali.

Aliyepokea tuzo hiyo kutoka kwa Rais Samia ni Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya TPA,  Dk. Elinami Minja aliyeambatana na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka hiyo,  Plasduce Mkeli Mbossa.

Kikao kazi hicho cha siku tatu kilichoanza leo kinafanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa AICC na unatarajiwa kumalizika siku ya Ijumaa.

Akizungumza wakati akifungua kikao kazi hicho,  alielezea umuhimu wa mashirika ya umma kutimiza wajibu wao ili kuchangia katika kuvutia wawekezaji zaidi nchini na kuongeza ufanisi wa mashirika hayo.

Katika hotuba hiyo, Rais Samia alitoa maelekezo kwa taasisi za umma kuhakikisha zinafanya kazi kwa ufanisi mkubwa na kwa mujibu wa sheria na taratibu, ili kuongeza tija na kuwavutia wawekezaji wa ndani na nje.

Alibainisha kuwa, ili Tanzania iweze kushindana katika soko la kimataifa, ni muhimu kuhakikisha kuwa bidhaa na huduma zinazozalishwa na mashirika ya umma zinakidhi viwango vya kimataifa.

Rais Samia alitoa mfano wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS), akisisitiza kuwa ni lazima shirika hili lihakikishe bidhaa zote zinazozalishwa nchini zinakidhi viwango vya kimataifa, na wakati huo huo, kuzilinda bidhaa za ndani dhidi ya ushindani usio wa haki kutoka bidhaa duni za nje.

Aliwataka TBS kuwa makini katika kusimamia viwango ili kuhakikisha kuwa bidhaa za Tanzania zinaweza kushindana vema katika masoko ya nje na ndani.

Aidha, Rais Samia aliihimiza Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kufanya kazi kwa weledi ili kuondoa malalamiko ya wawekezaji kuhusiana na kodi.

Aliwataka kuhakikisha kwamba mfumo wa kodi unakuwa rafiki kwa wawekezaji, jambo ambalo litasaidia kuvutia wawekezaji zaidi nchini. Aliongeza kuwa TRA inapaswa kuwa na utaratibu mzuri wa kusaidia wafanyabiashara wa ndani ili waweze kukuza biashara zao na kushindana katika soko la kimataifa.

Katika hotuba hiyo, Rais Samia pia aliwataka viongozi wa mashirika ya umma kuwa wabunifu na kufikiria njia za kuwekeza nje ya nchi, lakini akasisitiza kwamba kabla ya kufanya hivyo, ni lazima wawe na mpango madhubuti na kufanya utafiti wa kina.

Alikumbusha kuwa kuna baadhi ya mashirika ambayo yamepoteza fedha nyingi kwa kufanya uwekezaji usio na tija kwa sababu ya kutokufanya utafiti wa kutosha.

Rais Samia alitoa wito kwa viongozi hao wa mashirika ya umma kushirikiana na sekta binafsi ili kuimarisha uchumi wa nchi. Aliwahimiza kujadili namna ambavyo mashirika ya umma yanaweza kusaidia sekta binafsi kupata masoko mapya na kuongeza uzalishaji wa ndani.

Rais Samia aliwataka viongozi hao kuhakikisha wanatekeleza majukumu yao kwa uadilifu na uwazi, na kuhakikisha kuwa wanatumia rasilimali za umma kwa uangalifu ili kuleta maendeleo kwa taifa zima.

Aliwahimiza kuwekeza katika maeneo ambayo yana tija na ambayo yataongeza mapato kwa nchi, badala ya kufanya maamuzi ya kisiasa ambayo hayana tija kwa uchumi wa taifa.

Leave a Comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *