Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Taifa na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Fadhili Maganya, amepongeza Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha kwa utekelezaji mzuri wa mpango wa mikopo ya asilimia 10 kwa vijana, wanawake na watu wenye ulemavu.
Maganya amesema ameridhishwa na hatua zilizofikiwa na Manispaa hiyo, akisema imepiga hatua kubwa katika utoaji wa mikopo na utekelezaji wa miradi ya maendeleo ikilinganishwa na maeneo mengine nchini.

Amesema hayo Julai 27, 2026 katika mkutano wa ndani wa chama uliofanyika katika Chuo cha Uongozi cha Mwalimu Nyerere, baada ya kumuhoji Mkurugenzi wa Manispaa ya Kibaha, Dk. Rogers Shemwelekwa, kuhusu utekelezaji wa mikopo hiyo.
“CCM tunataka utekelezaji wa Ilani kwa vitendo, na hapa tumeona kazi inayofanyika yenye manufaa kwa Serikali na wananchi wa Manispaa ya Kibaha,” amesema Maganya.
Kwa upande wake, Dk. Shemwelekwa amesema Manispaa ya Kibaha hadi sasa imetoa zaidi ya Sh bilioni 2.1 kwa vikundi 400, huku wanufaika zaidi ya 3,000 wakinufaika na mikopo hiyo.
Amesema Manispaa hiyo inaendelea na maandalizi ya kutoa mikopo mingine katika mwaka wa fedha 2026/2027 ili kuwafikia wajasiriamali wengi zaidi.

Ameeleza kuwa kabla ya utoaji wa mikopo hiyo, alifanya ziara katika mitaa na kata mbalimbali kutoa elimu kwa wananchi kuhusu taratibu na vigezo vya kupata mikopo, hatua iliyosaidia kuongeza idadi ya waombaji na kuboresha marejesho.
Maganya amesema hatua hiyo ni mfano wa utekelezaji unaopaswa kuigwa na halmashauri nyingine nchini, huku akimtaka Mkurugenzi kuhakikisha wataalamu wanawafikia wananchi kutoa elimu zaidi ili kuondoa vikwazo vinavyowafanya baadhi kushindwa kufikia sifa za kupata mikopo.
Mbunge wa Kibaha Mjini, Silvestry Koka, amemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa uamuzi wa kuifanya Kibaha kuwa Manispaa, akisema hatua hiyo imechochea ukuaji wa maendeleo na kuongeza mapato ya eneo hilo.





