Tanzania imesisitiza mbele ya Kamati ya Urithi wa Dunia ya UNESCO kuwa mpango wa wananchi kuhama kwa hiari kutoka Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro unalenga kulinda utu, haki za binadamu na wakati huo huo kuhakikisha uendelevu wa uhifadhi.
Kauli hiyo imetolewa katika kikao cha 48 cha Kamati ya Urithi wa Dunia kinachoendelea jijini Busan, Korea Kusini, ambapo Tanzania imewasilisha matokeo ya tathmini iliyofanywa na Tume ya Rais kuhusu changamoto za ardhi, ongezeko la watu na uhifadhi katika Ngorongoro.
Katibu wa Tume ya Rais iliyofanya tathmini ya masuala ya ardhi katika Wilaya ya Ngorongoro, Thadei Aldo Kabonge, amesema tathmini hiyo ilifanyika kwa muda wa miezi saba baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kuteua Tume mbili kufuatia malalamiko ya jamii ya Wamasai kutoka Ngorongoro.

Amesema idadi ya watu katika eneo hilo imeongezeka kutoka takribani 8,000 mwaka 1959 hadi 100,793 mwaka 2022, huku ikitarajiwa kufikia 276,651 ifikapo mwaka 2050. Ongezeko hilo, amesema, limeongeza mahitaji ya ardhi na ushindani kati ya uhifadhi, utalii na maendeleo ya jamii.
Tathmini hiyo pia imebaini ongezeko la mifugo kutoka 261,723 mwaka 1960 hadi 715,466 mwaka 2022, pamoja na ongezeko la makazi kutoka 13,381 mwaka 2019 hadi 17,734 mwaka 2025.
Kabonge amesema hali hiyo imeendelea kuongeza shinikizo kwenye maeneo ya malisho na njia za wanyamapori, huku uwezo wa jamii kujitegemea kwa kutegemea mifugo pekee ukipungua.
Kwa mujibu wa Tume, mwaka 2022 kulikuwa na wastani wa TLU 3.5 kwa kila mtu, ikilinganishwa na kiwango cha mahitaji kinachokadiriwa kuwa TLU nane kwa mtu mmoja, huku kiwango hicho kikitarajiwa kushuka hadi 1.5 ifikapo mwaka 2050.





Aidha, Tume imebaini kuongezeka kwa migogoro kati ya binadamu na wanyamapori, ambapo watu 77 waliuawa na wanyamapori kati ya mwaka 2015 na 2025, wengine 274 kujeruhiwa na mifugo 1,450 kuuawa.
Kutokana na changamoto hizo, Tume imependekeza marekebisho ya mfumo wa kisheria unaosimamia Ngorongoro, ikieleza kuwa sheria ya mwaka 1959 imepitwa na wakati na inahitaji kuendana na mabadiliko ya sasa ya uhifadhi, mazingira, teknolojia na maendeleo ya jamii.
Pia imependekeza kutambuliwa kwa maeneo mbadala kwa wananchi watakaopenda kuhama kwa hiari, huku Serikali ikiwaandalia vifurushi vya fidia na kuweka mazingira bora ya maisha katika maeneo hayo.
Tume imesisitiza kuwa wananchi wanaotaka kubaki wataendelea kuishi na kufanya shughuli zao wakati Serikali ikiweka mipango ya maendeleo, huku wanaotaka kuhama kwa hiari wakipewa fursa hiyo.
Aidha, imependekeza kuandaliwa kwa mkakati maalumu wa elimu ya umma utakaohusisha jamii ya Wamasai na wadau wengine katika kila hatua ya utekelezaji wa mapendekezo hayo.








