Motisha kwa walimu na wanafunzi imechangia kuimarisha ufaulu katika mitihani ya taifa ya elimu ya msingi na sekondari katika shule za MHL, kwa mujibu wa uongozi wa shule hizo.
Mkurugenzi Mtendaji wa shule hizo, Anasima Mutembei, amesema hayo katika mahafali ya kidato cha nne ya Shule ya Sekondari Victory iliyopo Mkuranga, mkoani Pwani, na Shule ya St Mark’s iliyopo Mbagala, Dar es Salaam.
Amesema MHL ina shule nane, zikiwamo tano za sekondari na tatu za msingi, na imeweka mfumo wa motisha kwa walimu wanaofanikisha wanafunzi kufanya vizuri katika mitihani.
Amesema mwalimu ambaye mwanafunzi wake anapata daraja A katika somo analofundisha hupewa Sh20,000, huku anayefanikisha mwanafunzi kupata daraja B akilipwa Sh10,000.

Kwa upande wa wanafunzi, Mutembei amesema waliofanya vizuri au kuonyesha vipaji wakiwa darasa la saba wanaweza kupata nafasi ya kusoma bila ada kuanzia kidato cha kwanza hadi cha nne.
Aidha, wanafunzi wanaofanya vizuri kuanzia kidato cha kwanza hadi cha nne wanaweza kupata nafasi ya kusoma bure kidato cha tano na sita katika shule hizo. Wazazi wenye watoto zaidi ya mmoja katika shule za MHL pia hunufaika na punguzo la ada.
Mutembei amesema shule hizo zimeanza kutumia televisheni madarasani kusaidia ufundishaji na ujifunzaji, badala ya kutegemea zaidi ubao na chaki.
Ameongeza kuwa shule hizo zinawafundisha wanafunzi stadi za maisha na ujasiriamali ili waweze kujitegemea wanapokuwa nyumbani wakati wa likizo au baada ya kuhitimu. Amesema falsafa ya shule hizo imejikita katika elimu, malezi na nidhamu.
Mutembei ameishukuru Serikali kwa kutambua mchango wa shule binafsi katika sekta ya elimu.
Mgeni rasmi katika mahafali hayo, Mkurugenzi wa Hospitali ya Tumaini Mission na Mwenyekiti wa Vituo Binafsi vya Afya katika Manispaa ya Temeke, Dk. Elisha Mshote, amewapongeza walimu kwa juhudi zao na kuwataka wahitimu kuzingatia nidhamu na kuepuka vitendo vinavyoweza kuharibu maisha yao.
Amesema vijana wanahitaji nidhamu ili waweze kuaminika na jamii, huku akiwataka kutumia stadi za maisha walizojifunza shuleni kujipatia kipato.
Mshote pia ameahidi kuchangia vitanda viwili kwa ajili ya vyumba vya huduma za afya katika shule za Victory na St Mark’s, pamoja na televisheni moja kwa ajili ya kusaidia ujifunzaji.





