Aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Mkuranga, mkoani Pwani, Khadija Nassir Ally, amewaaga watumishi wa halmashauri hiyo na kuwaomba wananchi kumpa ushirikiano mkuu mpya wa wilaya hiyo, Mwinyi Ahmed Mwinyi, ili kuendeleza mafanikio yaliyopatikana.
Khadija amesema hayo wakati wa makabidhiano ya ofisi, akiwashukuru watumishi na wakazi wa Mkuranga kwa ushirikiano waliompa katika kipindi chake cha uongozi.
“Nawashukuru wakazi wote wa Mkuranga, wakiwamo watumishi. Nimeweza kufanya kazi kwa kushirikiana nao na kufanikisha ndoto za wananchi wa Mkuranga,” amesema.
Pia amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kumwamini na kumpa nafasi ya kuwatumikia wananchi katika uongozi wake.
Amesema wananchi wa Mkuranga hawana sababu ya kuwa na wasiwasi kwa kuwa wamepata kiongozi anayefanya kazi kwa bidii, akimtaja Mwinyi kuwa mtu mwenye uwezo wa kuendeleza shughuli za maendeleo wilayani humo.

“Mkuranga, mmepata mkuu wa wilaya jembe. Pale tulipokwama, Mwinyi ataendeleza,” amesema Khadija, huku akimkaribisha kuanza majukumu yake na kumweleza kuwa atakuta timu ya watumishi itakayomsaidia kutekeleza majukumu yake.
Ameongeza kuwa ahadi zilizotolewa na Rais Samia kwa wananchi wa Mkuranga zimetekelezwa kwa mafanikio, huku akisisitiza kuwa maendeleo ni mchakato unaohitaji ushirikiano wa viongozi na wananchi.
Kwa upande wake, Mkuu mpya wa Wilaya ya Mkuranga, Mwinyi Ahmed Mwinyi, amewaomba wananchi na watumishi kumpa ushirikiano ili kwa pamoja waendelee kuijenga wilaya hiyo.
Katibu Tawala wa Wilaya ya Mkuranga, Omary Said Mwanga, amesema Khadija ameitumikia wilaya hiyo kuanzia mwaka 2021 hadi 2026 na kumpongeza kwa ushirikiano aliouonyesha katika kipindi chake cha uongozi.
Hafla hiyo ya makabidhiano ilihudhuriwa na watumishi wa halmashauri, madiwani, viongozi wa dini na chama tawala, pamoja na wawakilishi wa makundi mbalimbali ya wananchi.





