Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), ameongoza kikao cha maandalizi ya Ushiriki wa Ujumbe wa Tanzania katika Mikutano ya Mwaka ya Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) na Benki ya Dunia (World Bank Group), inayofanyika jijini Bangkok nchini Thailand, kuanzia tarehe 12 hadi 18 Oktoba 2026, huku akisisitiza kuwa Tanzania imejipanga kikamilifu kunufaika na mikutano hiyo kiuchumi na kijamii.
Mhe. Balozi Omar amebainisha kuwa ushiriki wa Tanzania ni wa kimkakati kwa ajili ya uhamasishaji wa rasilimali na usimamizi wa fedha za nje nchini, kama mwanachama wa taasisi hizi, na kutumia fursa hiyo kufanya mazungumzo ya ngazi ya juu na viongozi wa taasisi hizo, ikiwemo Makamu wa Rais anayesimamia Kanda ya Kusini Mashariki mwa Afrika na wakurugenzi watendaji, ili kuendeleza ajenda za maendeleo.
“Moja ya maeneo muhimu yanayopewa kipaumbele ni utekelezaji wa mzunguko wa 21 wa IDA (IDA 21), ambayo Serikali imewasilisha orodha ya awali ya miradi inayotarajiwa kufadhiliwa na Benki ya Dunia na kuhakikisha kuwa miradi ya kipaumbele ya Taifa inapata ufadhili unaostahili” alisema Mhe. Balozi Omar.
Mbali na Benki ya Dunia, Tanzania inapanua wigo wa ushirikiano na wadau wengine wa maendeleo na inaendelea na mazungumzo na mashirika ya ukadiriaji wa mikopo kama Moody’s na Fitch, pamoja na kuvutia wakopeshaji wapya ili kuongeza fursa za upatikanaji wa fedha na kuimarisha imani ya wawekezaji kwa uchumi wa Tanzania.
Kwa ujumla, Serikali imesisitiza kuwa ushiriki wake katika mikutano hii si tu wa kuimarisha kidiplomasia ya kiuchumi, bali ni wa kiutendaji ili kuhakikisha kuwa kila fursa ya ufadhili inatumika ipasavyo, miradi inatekelezwa kwa viwango vinavyokubalika, na pale inapobidi, serikali itatafuta msaada wa kibajeti (GBS) ili kukidhi mahitaji ya rasilimali katika programu mbalimbali za maendeleo.
Awali, akitoa taarifa ya utekelezaji wa Majukumu ya Ubalozi wa Heshima nchini Thailand, Balozi wa Heshima wa Tanzania nchini humo Mhe. Florean Rwehumbiza, alieleza kuwa Ofisi yake inaendelea kuimarisha ushirikiano wa diplomasia ya kiuchumi kupitia uhusiano wa kibiashara, utalii, na huduma za afya kati ya nchi hizo mbili.
Alibainisha kuwa Ofisi yake imekuwa ikifanya kazi kubwa ya kutangaza utalii wa Tanzania katika nchi za Kusini-Mashariki mwa Asia, ikiwemo Malaysia, Vietnam, Cambodia, Lao, na Hong Kong, jitihada ambazo zimezaa matunda kwa kushawishi mashirika ya ndege kuanza safari za moja kwa moja kuelekea Tanzania, jambo linalolenga kurahisisha usafiri kwa watalii na wafanyabiashara.
Kuhusu sekta ya afya, Mhe. Rwehumbiza alisema kuwa Tanzania imekuwa nchi ya pili barani Afrika kwa kupeleka wagonjwa nchini Thailand kwa ajili ya matibabu ambapo Takwimu zinaonesha kuwa kuanzia Desemba mwaka jana hadi Juni mwaka huu, Watanzania wametumia taktiban pesa za Thailand (Thai Baht) milioni 150 kwa huduma za matibabu nchini humo.
Katika upande wa usafiri, alisisitiza kuwa Tanzania ndiyo nchi pekee katika ukanda wa Afrika Mashariki inayoruhusiwa kuingia Thailand bila kuhitaji kadi ya homa ya manjano (yellow fever card), mradi msafiri asipitie Nairobi, Aidha, ofisi hiyo inaendelea kupigania upatikanaji wa mfumo wa visa on arrival kwa wasafiri kutoka Tanzania ili kurahisisha zaidi mwingiliano wa watu.
Naye Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kidumu ya Bunge ya Bajeti, Mhe. Ali Hassan Omar, aliipongeza Wizara ya Fedha kwa kulishirikisha Bunge katika Vikao hivyo vya Mwaka vya IMF na Benki ya Dunia na namna Serikali inavyofanya jitihada za kuhakikisha Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2050 inatekelezwa kwa mafanikio kupitia upatikanaji wa rasilimali ferha na mipango mbalimbali ya kukuza uchumi.








Kikao hicho kilihudhuriwa pia na Waziri wa Fedha-Zanzibar, Mhe. Dkt. Juma Malik Akil (Mb), Naibu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bajeti ya Bunge, Mhe. Ali Hassan Omar (Mb), Mjumbe wa Kamati ya Bajeti ya Bunge, Mhe. Enock Zadock Koola (Mb), Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mlipaji Mkuu wa Serikali, Dkt. Natu El-Maamry Mwamba, Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Mipango, ambaye pia ni Katibu Mtendaji wa Tume ya Taifa ya Mipango, Dkt. Tausi Kida, Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Bw. Emmanuel Tutuba na Viongozi wengine waandamizi wa Serikali na baadhi ya Taasisi zake.




