Akizungumza wakati wa ziara yake ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa kituo hicho, Makamu wa Rais amesema Mkoa wa Rukwa wenye mahitaji ya takribani megawati 30, kwa sasa unapokea megawati 16 pekee, hali iliyokuwa ikikwamisha shughuli za uzalishaji, hususan uchakataji wa mazao ya kilimo na madini.
Amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imewekeza katika mradi huo ili kuhakikisha Rukwa inaunganishwa na Gridi ya Taifa na kuwa kitovu cha uzalishaji na biashara ya umeme katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kusini mwa Afrika.
“Leo hii TANESCO inanunua umeme Zambia, lakini kwa laini hii sisi tutaanza kuiuzia Zambia umeme mkubwa na wa uhakika,” amesema Makamu wa Rais, huku akiwataka wa wawekezaji kuchangamkia fursa za kiuchumi mkoani Rukwa na wananchi kulinda miundombinu hiyo.

Awali, Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Salome Makamba, amesema mradi huo ni sehemu ya uwekezaji wa Serikali unaodhihirisha dhamira ya dhati ya kuhakikisha mikoa yote nchini inaunganishwa na Gridi ya Taifa.
Amesema asilimia 90 ya wafanyakazi wanaotekeleza mradi huo ni Watanzania, huku akieleza kuwa majaribio ya mitambo yanatarajiwa kuanza katikati ya Novemba 2026.
Kukamilika kwa mradi huo kunatarajiwa kuondoa changamoto ya upungufu wa umeme, kuchochea ujenzi wa viwanda, kuongeza thamani ya mazao na kufungua fursa mpya za ajira na uwekezaji, huku Tanzania ikiimarisha nafasi yake katika biashara ya nishati kikanda.






