Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha St. Augustine Tanzania (SAUT), jijini Mwanza, wanatarajia kupunguza changamoto za kiusalama wanapokwenda mabwenini na maeneo mengine ya chuo nyakati za usiku, baada ya kufungwa kwa taa 214 za sola katika mtandao wa barabara wenye urefu wa kilomita 6.42.
Mradi huo unaofadhiliwa na Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA), unalenga kuimarisha usalama wa wanafunzi zaidi ya 13,600, watumishi wa chuo na jamii inayozunguka taasisi hiyo, huku mwanga huo ukitarajiwa kurahisisha shughuli za kujifunza na kutembea usiku.
Mkurugenzi wa Teknolojia za Nishati Jadidifu na Mbadala wa REA, Mhandisi Advera Mwijage, ameyasema hayo alipotembelea chuo hicho kukagua maendeleo ya mradi, kuwa uwekaji wa taa hizo umezingatia mahitaji ya taasisi zinazohudumia idadi kubwa ya watu.
Amesema kabla ya mradi huo, wanafunzi walikabiliwa na changamoto za kiusalama wanapotembea kuelekea mabwenini nyakati za usiku, zikiwamo kuvamiwa na kupokonywa vifaa vya kielektroniki kama kompyuta mpakato na simu.
“Katika chuo hiki cha SAUT, tumefunga taa 214 kwenye mtandao wa barabara wenye urefu wa kilomita 6.42. Tumeshuhudia uhitaji mkubwa sana hapa kwa sababu hapo awali wanafunzi walikuwa wakikabiliwa na changamoto kubwa ya kiusalama,” amesema Mhandisi Advera .
Amesema mradi huo ni sehemu ya programu za REA zinazolenga kupanua upatikanaji wa nishati, zikiwamo kusambaza umeme vijijini, kuwezesha sekta binafsi kuzalisha umeme, kukuza matumizi ya nishati safi ya kupikia na kuimarisha huduma za taa katika taasisi zinazohudumia jamii.
Makamu Mkuu wa Chuo hicho, Profesa Sr. Clara Rupia, amesema taa hizo zitakuwa na mchango mkubwa katika shughuli za kila siku za wanafunzi na watumishi, kutokana na ratiba ya masomo kuendelea hadi nyakati za usiku.
Amesema chuo huendesha masomo kuanzia saa moja asubuhi hadi saa tatu usiku, hivyo mwanga huo utarahisisha wanafunzi kutembea kati ya madarasa na mabweni.
Naye msimamizi wa ufundi wa mradi huo, ambaye pia ni Mkurugenzi wa Fedha wa SAUT, Fr. Cletus Uhinga, amesema kati ya taa hizo, takribani asilimia 60 hadi 65 zilikuwa tayari zimefungwa na kuanza kutumika wakati wa ukaguzi huo.
Mradi huo una thamani ya Sh milioni 820.6, ambapo Serikali kupitia REA imechangia Sh milioni 793.8 na SAUT imetoa Sh milioni 32.6.




