Wateja wa Gesi Asilia Iliyoshindiliwa (CNG) wanaweza kukabiliwa na mabadiliko ya bei ya nishati hiyo baada ya Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) kuanza mchakato wa kupitia upya viwango vya bei na faida kwa watoa huduma, huku wadau wakitaka maslahi ya wananchi yazingatiwe ili kuendeleza matumizi yake.
Kwa sasa, kilo moja ya CNG inauzwa kwa Sh 1,550 jijini Dar es Salaam, lakini EWURA imesema mapitio hayo yanalenga kuzingatia gharama halisi za uendeshaji, mabadiliko ya thamani ya fedha za kigeni na gharama za kusafirisha gesi katika maeneo mbalimbali nchini.
Akizungumza jijini Dar es Salaam, Mhandisi wa Gesi Asilia wa EWURA, Selemani Chombo, aliyemwakilisha Mkurugenzi wa Idara ya Gesi Asilia, amesema mchakato huo unahusisha kukusanya maoni ya wadau kabla ya kutangaza viwango vipya vya bei.
Amesema ongezeko la matumizi ya CNG na kusambaa kwa huduma hiyo katika maeneo ya Morogoro, Kibaha, Mtwara na Ruvuma kunahitaji mfumo wa upangaji bei unaozingatia gharama za kufikisha gesi kwa watumiaji katika kila eneo.
Amefafanua kuwa tofauti ya umbali kutoka kwenye chanzo cha gesi na gharama za usafirishaji zinaweza kusababisha bei kutofautiana kati ya maeneo.




Chombo amesema EWURA inataka kuweka uwiano kati ya maslahi ya watoa huduma na watumiaji, ili biashara ziweze kuendelea kwa uendelevu huku wananchi wakipata gesi kwa bei wanayoweza kumudu.
Katika semina hiyo ya siku mbili ya wadau wa sekta ya gesi asilia, iliyolenga pia kujadili usalama wa uendeshaji na matumizi ya CNG, wadau wameeleza mitazamo tofauti kuhusu mapendekezo ya mabadiliko ya bei.
Mwakilishi wa kampuni ya Tembo Energies, Prasanna, amesema ongezeko la haraka la bei ya CNG linaweza kupunguza kasi ya wananchi kuhamia kwenye matumizi ya nishati hiyo, hivyo akaitaka Serikali kuzingatia umuhimu wa bei himilivu.
Amesema licha ya gharama kubwa za uwekezaji na faida ndogo kwa waendeshaji wa vituo, ni muhimu kuweka mbele maslahi ya wananchi na ukuaji wa soko la gesi asilia.
Ameeleza kuwa kampuni hiyo imekuwa ikiendesha kituo kikuu cha kujaza CNG jijini Dar es Salaam kwa miezi 26 na wakati wa mahitaji makubwa huhudumia zaidi ya magari 1,000 kwa siku.
Amesema utulivu wa bei kwa takribani miaka 15 umechangia kuvutia wananchi kutumia CNG, hasa ikilinganishwa na mafuta ya petroli na dizeli ambayo bei zake huathiriwa na mabadiliko ya uchumi wa dunia.
Prasanna ameongeza kuwa kampuni hiyo ina mpango wa kuwekeza katika mradi mdogo wa Gesi Asilia Iliyoyeyushwa (Mini LNG) mkoani Mtwara, utakaosaidia kufikisha gesi katika maeneo mbalimbali, yakiwemo Dodoma, Mwanza na Mbeya.
Pia ameiomba Serikali kuimarisha uwazi katika mfumo wa kupanga na kulipia gesi kwa kutumia Shilingi za Tanzania katika kuwasilisha gharama, badala ya kutegemea mabadiliko ya thamani ya Dola ya Marekani.




Usalama wa magari ya CNG
Mbali na suala la bei, wadau wameeleza umuhimu wa kuimarisha usalama wa magari yanayotumia CNG, hususan yanayosafirisha abiria.
Mkaguzi wa magari yanayotumia gesi asilia kutoka Shell Engineering, Baraka Godfrey Majembe, amesema elimu kuhusu ubora na usalama wa matumizi ya gesi ni muhimu kutokana na kuongezeka kwa magari yanayotumia nishati hiyo.
Amesema ni muhimu kuhakikisha ukaguzi na usimamizi wa magari hayo unazingatia usalama ili kuzuia vihatarishi vinavyoweza kuhatarisha maisha ya abiria na watumiaji wengine wa barabara.
Kwa upande wake, Meneja wa EWURA Kanda ya Mashariki, Lorivii Longidu, aliyemwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa mamlaka hiyo, amesema EWURA ina jukumu la kusimamia usalama wa miundombinu, ubora wa huduma na upatikanaji wa gesi kwa bei stahiki.
Amesema sheria zimeipa EWURA mamlaka ya kudhibiti shughuli za mkondo wa kati na wa chini wa sekta ya gesi asilia, ikiwemo uchakataji, usafirishaji, uhifadhi na usambazaji.
Ameeleza kuwa hadi Oktoba 2026, EWURA ilikuwa imetoa leseni 22 kwa watoa huduma za CNG na vibali 10 vya ujenzi wa miundombinu hiyo vilikuwa katika hatua mbalimbali za utekelezaji.
Aidha, mamlaka hiyo imetoa leseni nne za uendeshaji wa vituo vya gesi kwa matumizi ya nyumbani katika mikoa ya Mtwara, Pwani, Kigoma na Dar es Salaam, pamoja na leseni 11 za kusambaza gesi asilia iliyogandamizwa kwa kutumia magari.
Longidu amesema EWURA imeboresha mfumo wa kielektroniki wa maombi ya vibali vya ujenzi na leseni kupitia EWURA e-Services, unaowawezesha waombaji kupata huduma bila kufika katika ofisi za mamlaka hiyo.
Amehimiza wadau kutumia semina hiyo kutoa maoni kuhusu mapendekezo ya viwango vya bei na faida, akisema yatasaidia mamlaka kufanya maamuzi yanayozingatia maslahi ya watoa huduma na watumiaji.








