Uwekezaji katika majengo ya kibiashara, nyumba na viwanja ni miongoni mwa maeneo ambayo Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) unayatumia kushiriki katika sekta ya majengo na uwekezaji wa ardhi, huku ukilenga kutoa fursa kwa wanachama na wananchi.
Maelezo hayo yametolewa na Afisa Mwandamizi wa Idara ya Uwekezaji, Milki na Usimamizi wa Majengo wa PSSSF, Arnold Kagaruki, wakati wa Kongamano na Maonesho ya Sekta ya Majengo na Uwekezaji wa Ardhi (TAREX 2026), yanayofanyika kwa siku tatu jijini Dar es Salaam.
Kagaruki amesema ushiriki wa PSSSF katika maonesho hayo unatokana na nafasi yake kama mdau wa sekta hiyo kupitia uwekezaji katika miradi mbalimbali ya majengo na ardhi nchini.
Ameeleza kuwa, pamoja na uwekezaji katika majengo ya kibiashara, nyumba na viwanja, Mfuko unatekeleza uwekezaji wa kimkakati kwa kushirikiana na Kituo cha Mikutano cha Kimataifa Arusha (AICC) kujenga Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Mount Kilimanjaro jijini Arusha, ambacho ujenzi wake umeanza.
Akizungumza katika banda la PSSSF, Waziri Mkuu, Dk. Mwigulu Nchemba, ambaye alikuwa mgeni rasmi wa kongamano hilo, ameipongeza taasisi hiyo kwa usimamizi wa shughuli zake na utekelezaji wa majukumu yake.
“Hongereni sana, natambua kazi nzuri mnayofanya. Endeleeni hivyo hivyo,” amesema Waziri Mkuu.
Kagaruki amesema kupitia jukwaa hilo, PSSSF inalenga kutangaza fursa zinazotokana na uwekezaji wake, kuimarisha mahusiano na wadau wa sekta ya majengo na ardhi, pamoja na kutoa elimu kwa wananchi kuhusu shughuli na huduma za Mfuko.
Kongamano na maonesho hayo yanawakutanisha waendelezaji wa miradi ya majengo, wawekezaji, taasisi za kifedha, mamlaka za udhibiti na watoa huduma za kitaalamu kutoka Tanzania Bara, Zanzibar na Kenya.








