Wakazi na wafanyabiashara wa mikoa ya Mbeya na Songwe wameanza kurejea katika shughuli zao baada ya huduma ya umeme kurejeshwa usiku wa kuamkia Novemba 23, 2026, kufuatia kukatika kwake kulikosababishwa na kuanguka kwa mnara wa njia ya kusafirisha umeme eneo la Inyala.
Baadhi ya wananchi wameeleza kufurahishwa na kurejea kwa huduma hiyo, wakisema kukatika kwa umeme kuliathiri biashara na shughuli nyingine zilizotegemea nishati hiyo.
Mkazi wa Soweto, Victor Mkini, ameishukuru Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kwa juhudi za kufanya kazi usiku na mchana kurejesha huduma hiyo.
Amesema shirika hilo lilikuwa likiwapatia taarifa kuhusu hatua zilizokuwa zikichukuliwa hadi umeme uliporejea.




Kwa upande wake, Lilian Kalugha amesema kukatika kwa umeme kuliathiri shughuli zake za biashara, ambazo zinategemea zaidi huduma hiyo, huku akilishukuru TANESCO kwa kuendelea kutoa taarifa na ushirikiano wakati wa changamoto hiyo.
Naye Hekima Kadogo amesema kukatika kwa umeme kulisimamisha shughuli mbalimbali, lakini utoaji wa taarifa kuhusu maendeleo ya jitihada za kurejesha huduma ulimsaidia kufahamu hatua zilizokuwa zikichukuliwa.
Umeme ulikatika baada ya kuanguka kwa mnara wa njia mpya ya kusafirisha umeme ya kilovolti 400 ya Mradi wa TAZA katika eneo la Inyala, Novemba 21, 2026.
Tukio hilo liliathiri pia miundombinu ya njia ya kilovolti 220 inayosafirisha umeme kutoka Iringa kwenda Mbeya.
Kufuatia tukio hilo, TANESCO ilifanya kazi usiku na mchana kurejesha huduma, hatua iliyowezesha umeme kurejea katika mikoa ya Mbeya na Songwe usiku wa kuamkia Novemba 23, 2026.








