HomeBiasharaCRDB, TANESCO kuweka mkakati wa kuunganisha kaya milioni 8.3

CRDB, TANESCO kuweka mkakati wa kuunganisha kaya milioni 8.3

KAYA zenye kipato cha chini vijijini zinatarajiwa kunufaika na ruzuku ya Sh27,000 kwa ajili ya kuunganishiwa umeme kupitia programu ya iMBEJU Nuru, inayotekelezwa na CRDB Bank Foundation kwa kushirikiana na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO).

Mpango huo umepokelewa na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, ambayo imeeleza kuwa utasaidia kuongeza kasi ya upatikanaji wa umeme na kuchochea maendeleo ya kiuchumi katika jamii za vijijini.

Programu hiyo inalenga kusaidia kuunganisha kaya 510,000 kwa mwaka, ikiwa ni sehemu ya mchango katika Mpango wa Taifa wa Nishati (M300), unaolenga kuunganisha kaya mpya milioni 8.3 na kuongeza kiwango cha upatikanaji wa umeme hadi asilimia 75 ya kaya nchini ifikapo mwaka 2030.

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Subira Mgalu, amesema mpango huo utaongeza fursa kwa wananchi wenye kipato cha chini kupata huduma ya umeme kupitia ruzuku na mikopo yenye masharti nafuu.

Akiwasilisha taarifa kuhusu mpango huo, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Dk. Abdulmajid Nsekela, amesema benki hiyo itaendelea kushirikiana na Serikali kufadhili miradi ya kimkakati inayochochea ukuaji wa uchumi, kuvutia uwekezaji na kuboresha maisha ya wananchi.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB Bank Foundation, Tully Esther Mwambapa, amesema kila kaya ya kijijini yenye uhitaji itapata ruzuku ya Sh27,000 kwa ajili ya gharama za kuunganishiwa umeme.

Amesema fedha hizo zitalipwa moja kwa moja kwa TANESCO baada ya mhusika kuwasilisha maombi na kukidhi vigezo vya mpango huo.

Ameongeza kuwa kaya zitakazohitaji huduma zaidi, ikiwamo kusambaza umeme katika maeneo mengine ya makazi au kwenye miradi ya uzalishaji kipato, zitaweza kupata mikopo yenye riba ya asilimia 10.

Kwa mujibu wa Tully, utaratibu wa kurejesha mikopo hiyo utahusishwa na ununuzi wa umeme kupitia mfumo wa LUKU, ambapo mteja atakatwa kiasi cha marejesho kila anaponunua umeme.

“Mkopo huu nafuu utarejeshwa kwa njia rahisi kabisa; mteja atakatwa kila anaponunua LUKU,” amesema.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Nishati, Salome Makamba, amesisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi katika kuongeza upatikanaji wa nishati, kuchochea shughuli za kiuchumi na kuunga mkono utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

RELATED ARTICLES

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisment -
NMB Tanzania

Most Popular

Recent Comments