Katika jitihada za kuimarisha uwezo wa taasisi zinazowahudumia wajasiriamali nchini, CRDB Bank Foundation imeendesha mafunzo maalumu kwa maafisa wa Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO), Wakala wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi Zanzibar (ZEEA) na watendaji wa Serikali za Mitaa kutoka mikoa ya Mwanza, Tanga na Pemba.
Mafunzo hayo ni sehemu ya utekelezaji wa mradi wa Inclusive Financial Services for Women and Youth-led MSMEs (IncluCities Project SASA) unaolenga kuongeza upatikanaji wa huduma za fedha na fursa za maendeleo kwa wanawake na vijana wajasiriamali.
Akifungua mafunzo hayo ya siku tatu, Mkuu wa Kitengo cha Huduma kwa Wakulima wa Benki ya CRDB, Shaaban Maregesi, amesema mafunzo hayo yameandaliwa kufuatia tathmini iliyobaini kuwa, licha ya taasisi hizo kuwa na watumishi wenye uzoefu na mifumo imara ya utendaji, bado kuna maeneo yanayohitaji kuimarishwa ili kuongeza ubora wa huduma kwa wananchi.


Ametaja maeneo hayo kuwa ni ushauri wa ujasiriamali, usimamizi wa fedha, tathmini ya biashara ndogo na za kati (SME Appraisal), huduma bora kwa wateja pamoja na matumizi ya mifumo ya kidijitali.
“Kuna fursa kubwa ya kuendelea kuimarisha uwezo wa taasisi hizi ili ziweze kuwahudumia wananchi kwa ufanisi zaidi na kuwasaidia kukuza biashara zao,” amesema Maregesi.
Mradi wa IncluCities Project SASA unatekelezwa kwa ushirikiano kati ya CRDB Bank Foundation na taasisi ya maendeleo ya kimataifa ya Enabel. Hadi sasa umewafikia zaidi ya wananchi 200 katika mikoa ya Tanga, Mwanza na Pemba, huku zaidi ya wajasiriamali 50 wakinufaika na mitaji wezeshi yenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 400.
Maregesi amesema lengo la CRDB Bank Foundation ni kuhakikisha taasisi zinazotoa huduma kwa wanawake na vijana zinakuwa na uwezo mkubwa zaidi wa kuwawezesha kuingia katika uchumi rasmi, kukuza biashara zao na kupata huduma za kifedha kwa urahisi.

“Mafanikio ya wanawake na vijana wajasiriamali yanategemea kwa kiasi kikubwa uwezo wa taasisi zinazowazunguka kuwapa huduma bora, sahihi na kwa wakati. Ndiyo maana tunaendelea kuwekeza katika kuzijengea uwezo taasisi hizi,” amesema.
Washiriki wa mafunzo hayo wanatarajiwa kupata ujuzi katika maeneo sita muhimu ambayo ni maendeleo ya ujasiriamali, usimamizi wa fedha, utawala bora na uongozi wa taasisi, tathmini ya biashara ndogo na za kati, huduma kwa wateja na matumizi ya teknolojia za kidijitali katika kuboresha utoaji wa huduma.
Kwa mujibu wa CRDB Bank Foundation, ushirikiano wake na SIDO, ZEEA, Serikali za Mitaa na Enabel unalenga kujenga mazingira bora kwa wajasiriamali, kuongeza ajira na kukuza uchumi jumuishi nchini.
Mbali na mradi huo, taasisi hiyo imeendelea kushirikiana na Serikali kupitia programu mbalimbali za uwezeshaji, ikiwemo Inuka na Uchumi wa Buluu Zanzibar, pamoja na kutoa dhamana za mikopo kwa wajasiriamali wanaopata mafunzo kupitia SIDO.
Mafunzo hayo yanatarajiwa kuboresha huduma zinazotolewa na taasisi washirika, kuongeza ushirikiano kati yao na kuwawezesha wanawake na vijana kutumia kikamilifu fursa za kiuchumi zilizopo kwa ajili ya kukuza biashara, ajira na kipato.






