BENKI ya NMB imezindua dawati maalumu la kuwahudumia wateja wenye ulemavu, likiwa na huduma ya mawasiliano ya video inayosaidiwa na wakalimani wa lugha ya alama ili kurahisisha upatikanaji wa huduma za kibenki.
Dawati hilo limeanzishwa katika Kituo cha Mawasiliano cha benki hiyo na linawalenga wateja wenye ulemavu wa kusikia, kuona na viungo, kwa lengo la kupunguza vikwazo vya mawasiliano na kuongeza ushiriki wao katika huduma za kifedha.
Wateja wanaweza kupata msaada kupitia namba ya simu ya bure 0800 002002, huduma ya video kupitia WhatsApp inayosaidiwa na wakalimani wa lugha ya alama, pamoja na matawi ya benki hiyo nchini.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa Wiki ya Huduma kwa Wateja 2026 jijini Dar es Salaam, Afisa Mkuu wa Wateja Binafsi na Biashara wa NMB, Filbert Mponzi, amesema huduma hiyo inalenga kuhakikisha watu wenye ulemavu wanapata huduma za kibenki kwa heshima na usawa.
Amesema pia dawati hilo litasaidia kulinda faragha za wateja na kupunguza utegemezi wao kwa watu wengine wanapohitaji huduma za kibenki.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Shirikisho la Vyama vya Watu Wenye Ulemavu Tanzania (SHIVYAWATA), Nemes Temba, ameipongeza benki hiyo kwa hatua hiyo, akisema itasaidia kuondoa vikwazo vya mawasiliano na kuwawezesha watu wenye ulemavu kushiriki kikamilifu katika matumizi ya huduma za kifedha nchini.




