HomeHabariREA yaeleza maendeleo ya mradi wa umeme wa maji Ludewa

REA yaeleza maendeleo ya mradi wa umeme wa maji Ludewa

SERIKALI kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) imetoa zaidi ya Sh738 milioni kwa awamu ya pili ya kuendeleza mradi wa umeme unaotumia maporomoko ya maji katika Kijiji cha Boimanda, Wilaya ya Ludewa, mkoani Njombe.

Mradi huo wenye uwezo wa kuzalisha kilowati 317 unasimamiwa na Shirika la Masista wa Benedictine la Kanisa Katoliki, ukiwa na lengo la kuongeza upatikanaji wa umeme na kuchochea shughuli za kiuchumi na kijamii katika maeneo yanayozunguka mradi.

Mkurugenzi wa Nishati Jadidifu na Teknolojia Mbadala wa REA, Mhandisi Advera Mwijage, amesema hayo wakati wa kutembelea na kukagua maendeleo ya mradi huo.

Amesema sehemu kubwa ya miundombinu imekamilika, ikiwamo jengo la kufungia mitambo ya kuzalisha umeme, huku kazi iliyobaki ikiwa ni kukamilisha miundombinu ya kuunganisha umeme unaozalishwa na mfumo wa TANESCO ili uweze kuingizwa katika gridi ya taifa.

Mwijage amewataka wananchi wanaoishi katika maeneo yanayozunguka mradi huo kutunza mazingira na kulinda vyanzo vya maji, akisisitiza kuwa upatikanaji wa maji ya kutosha ni muhimu kwa uendelevu wa uzalishaji wa umeme.

Kwa upande wake, msimamizi wa mradi huo kutoka Shirika la Masista wa Benedictine, Sister Imakulata Mlowe, amesema shirika hilo limepokea zaidi ya Sh4.5 bilioni kutoka Serikali kupitia REA kwa ajili ya ujenzi na maendeleo ya mradi.

Amesema fedha hizo zimetumika kujenga bwawa, jengo la mitambo ya kuzalisha umeme (power house) pamoja na miundombinu ya kusambaza umeme kwa wakazi wa vijiji vya Boimanda na Matola.

Mlowe amesema mradi utakapokamilika, utasaidia kuboresha huduma za afya na maji, kuongeza mwanga wa uhakika na kuwawezesha wananchi kuanzisha au kupanua shughuli za biashara, zikiwamo saluni na matumizi ya mashine mbalimbali zinazohitaji umeme.

Mradi huo ni sehemu ya juhudi za Serikali za kuongeza uzalishaji wa umeme kupitia nishati jadidifu na kupanua upatikanaji wa nishati katika maeneo ya vijijini.

RELATED ARTICLES

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisment -
NMB Tanzania

Most Popular

Recent Comments