HomeHabariOSHA yagusa maisha ya wakazi wa Kilimanjaro

OSHA yagusa maisha ya wakazi wa Kilimanjaro

Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) umegusa maisha ya wananachi wa Mkoa wa Kilimanjaro kupitia kampeni yake ya huduma kwa jamii ambapo imekabidhi vifaa vya msaada katika mashule, hospitali pamoja na kutoa mafunzo ya usalama na afya kwa wajasiriamali wadogo zaidi ya 500.

Makundi yaliyonufaika na kampeni hiyo ni kutoka Wilaya za Mwanga na Moshi Mjini ambapo OSHA imepanda miti 200 ya matunda katika shule mbalimbali za msingi na sekondari ndani ya Wilaya ya Mwanga.

Aidha, imekabidhi mashuka 100 katika Hospitali ya Wilaya ya Mwanga, vifaa vya michezo pamoja na kutoa mafunzo ya usalama na afya yaliyofanyika sambamba na kukabidhi vifaa kinga kwa makundi ya wajasiriamali wadogo wenye ulemavu pamoja na maafisa usafirishaji (bodaboda).

Akizungumza katika kilele cha kampeni hiyo katika Viwanja vya Chuo cha Polisi Moshi, Mgeni Rasmi wa Bonanza la OSHA la Huduma kwa Jamii (OSHA CSR Bonanza 2026) ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Siha, Dkt. Christopher Timbuka, amesema lengo la kampeni hiyo ni kugusa maisha ya makundi yenye mahitaji maalum katika jamii.

“Miongoni mwa makundi yaliyonufaika na kampeni hii ni pamoja na Maafisa Usafirishaji (Bodaboda) 200 wa Wilaya ya Mwanga na Moshi, Wanachama 70 kutoka Shirikisho la Vyama vya Watu Wenye Ulemavu (SHIVYAWATA),  Shule za Sekondari Mwanga pamoja na Hospitali ya Wilaya ya Mwanga.” 

Mtendaji Mkuu wa OSHA, Bi. Khadija Mwenda, amesema tukio hilo ni utekelezaji wa mkakati wa OSHA wa kurudisha kwa jamii sambamba na utekelezaji wa majukumu yake ya msingi ya kusimamia uzingatiaji wa kanuni bora za usalama na afya katika maeneo ya kazi nchini.

“Jukumu letu kubwa ni kuhakikisha maeneo ya kazi yanakuwa na mifumo madhubuti ya kuwalinda wafanyakazi dhidi ya vihatarishi vya ajali, magonjwa na vifo mahali pa kazi. Sambamba na utekelezaji wa majukumu yetu, tumekuwa na desturi ya kuwa na shughuli zinazogusa maisha ya watu katika kipindi ambacho tunashiriki mashindano ya SHIMIWI,” ameeleza Kiongozi Mkuu wa OSHA.

Kwa upande wake Katibu Tawala wa Wilaya ya Mwanga Mpampalika Mfaume pamoja na wanufaika wa kampeni hiyo, wameishukuru Taasisi ya OSHA kwa kubana matumizi yake ili kuwezesha upatikanaji wa mahitaji ya msingi kwa makundi mbalimbali ya jamii.

“Nimefurahia mafunzo ya leo kwasababu nimefahamu kazi za OSHA na zaidi nimejifunza kwamba usalama si tu kwa wafanyakazi walioajiriwa bali hata kwetu sisi tuliojiajiri tunatakiwa kuzingatia kanuni bora za usalama na afya kwa ajili ya usalama wetu wenyewe,” ameeleza Bi. Judika Allen Mshiriki wa Mafunzo.

Kampeni hiyo ya OSHA ya huduma kwa jamii ambayo imekuwa ikifanyika kila mwaka kama sehemu ya ushiriki wa Taasisi katika mashindano ya Shirikisho la Michezo ya Wizara, Idara na Wakala za Serikali (SHIMIWI), imehitimishwa kwa Bonanza OSHA la Huduma kwa Jamii (OSHA CSR Bonanza 2026) lililofanyika katika Viwanja vya Chuo cha Polisi Moshi Oktoba 08, 2026.

RELATED ARTICLES

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

- Advertisment -
NMB Tanzania

Most Popular

Recent Comments