Chama cha Waajiri Tanzania (ATE) kimezindua rasmi Tuzo za Mwajiri Bora wa Mwaka 2026 (EYA 2026) kwa mfumo mpya wa kidigitali ulioboreshwa unaolenga kuendana na mabadiliko ya dunia ya kazi pamoja na kuongeza uwazi, ushirikishwaji na ushindani wa haki kwa waajiri nchini.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mkurugenzi Mtendaji wa ATE, Adv. Suzanne Ndomba-Doran amesema kwa zaidi ya miaka 20, EYA imekuwa jukwaa muhimu la kutambua taasisi zinazowekeza katika ustawi wa wafanyakazi, kujenga mazingira bora ya kazi na kuendesha biashara kwa uwajibikaji na maadili.
Amesema mwaka jana ATE ilisimamisha kwa muda utoaji wa tuzo hizo ili kufanya tathmini ya kina kuhusu ufanisi wa programu hiyo katika kuendana na kasi ya mabadiliko ya mazingira ya kazi duniani.
“Tuliamua kutafakari upya mfumo wa EYA kwa kushirikisha wanachama, wataalamu na wadau mbalimbali ili kuhakikisha programu hii inaendelea kuwa na thamani na mchango mkubwa kwa waajiri nchini,” amesema.


Ameeleza kuwa tathmini hiyo ilionesha kuwa EYA bado inaaminika na kusaidia kuboresha usimamizi wa rasilimali watu, uwazi na uzingatiaji wa sheria za kazi, lakini pia wadau walipendekeza maboresho kadhaa ikiwemo kuongeza uwazi wa mchakato, kufanya mfumo kuwa jumuishi zaidi na kuifanya EYA kuwa chombo cha kujifunza mwaka mzima badala ya tukio la siku moja.
Aidha, amesema mapema mwezi Mei mwaka huu, ATE iliandaa warsha maalum katika Hoteli ya Four Points by Sheraton jijini Dar es Salaam iliyowakutanisha wadau mbalimbali kujadili mapendekezo ya maboresho ya mfumo wa EYA.
Kwa mujibu wa CEO huyo, mapendekezo yaliyotolewa ni pamoja na kuifanya EYA kuwa chapa maalum ya kitaifa, kuanzisha tovuti maalum ya EYA, kuboresha vigezo vya tathmini, kutumia wataalamu huru na kuanzisha tuzo za kisekta.
“EYA sasa si tukio la kawaida tena, bali ni chapa ya kitaifa inayoweka viwango vya ajira bora na kuhamasisha mageuzi katika maeneo ya kazi,” amesema.




Katika maboresho hayo, mfumo mpya wa tathmini utaangalia maeneo mbalimbali ikiwemo uongozi na utawala, utamaduni wa shirika, usawa na ujumuishaji, matumizi ya teknolojia katika rasilimali watu, afya na ustawi wa wafanyakazi, usalama mahali pa kazi, pamoja na ubunifu na tija.
Pia kwa mara ya kwanza, EYA 2026 itakuwa na tuzo za kisekta ili kuhakikisha mashirika yanashindana ndani ya sekta zao badala ya kulinganisha taasisi zenye mazingira tofauti ya kazi.
Amesema ATE pia imeongeza ushirikishwaji kwa biashara ndogo na za kati (SMEs) pamoja na sekta isiyo rasmi kwa kuanzisha makundi mapya ya tuzo ikiwemo SME Iliyoboreshwa Zaidi, Mwajiri Chipukizi wa Mwaka na Ubunifu Bora wa HR kwa SMEs.
Kwa upande wa sekta isiyo rasmi, amesema waendeshaji wa biashara ndogo sasa watapata nafasi ya kutambuliwa kwa mchango wao katika ustawi wa wafanyakazi, ubunifu, maadili ya kazi na maendeleo ya jamii.
Aidha, amesema mchakato wa tathmini umeimarishwa zaidi kwa kuhusisha tathmini huru za kitaalamu, tafiti za wafanyakazi, ukaguzi wa mazingira ya kazi na maamuzi ya jopo huru ili kuhakikisha kila ushindi unajengwa katika ushahidi na uhalisia.
CEO huyo amesisitiza kuwa EYA 2026 inalenga kuwa safari ya mwaka mzima ya kujifunza, kubadilika na kuboresha mazingira ya kazi nchini.
Amewataka waajiri wote nchini, kuanzia kampuni kubwa hadi biashara ndogo, kushiriki katika mpango huo kwa lengo la kujitathmini, kujifunza na kuchangia ujenzi wa mazingira bora ya kazi Tanzania.
“Nguvu ya uchumi wa nchi yoyote hutegemea ubora wa mazingira ya kazi na namna watu wanavyothaminiwa. EYA 2026 ni ahadi yetu ya kuinua viwango hivyo kila siku,” amesema.





